Ibn ´Uthaymiyn anakataza kutumia dawa za kuzuia hedhi kutokana na madhara yake

Swali: Ni ipi hukumu mwanamke kutumia dawa za kuzuia hedhi ili aweze kufunga mwezi mzima wa Ramadhaan?

Jibu: Asitumii tembe hizi. Zina madhara sana. Hilo limethibiti kwetu kupitia maneno ya madaktari. Madaktari ndio wanaotakiwa kurejelewa katika mambo haya. Wanataja madhara mengi. Kwa ajili hiyo watoto tumboni wenye kuzaliwa na muumbuko wamekuwa wengi kwa wanawake; ni wengi wenye kusema kwamba mtoto hana fuvu, hana mkono, hana mguu na mengineyo. Haya nimeambiwa na baadhi ya madaktari waaminifu kwamba miongoni mwa sababu zake ni kwa sababu ya kula tembe hizi. Kwa ajili hiyo nasema kwamba mwanamke asile chochote katika hayo. Akisema kwamba atapitwa na swawm na swalah. Tunamuuliza yamepita kwa amri ya nani? Ni kwa amri ya Allaah (´Azza wa Jall). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwa ´Aaishah akamkuta yuko analia wakati wa hajj ya kuaga kabla ya kufika Makkah, ´Aaishah wakati huo alikuwa ni mwenye kuhirimia ´Umrah ambapo akapata hedhi njiani, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaingia kwkae na akamkuta analia, akamuuliza kilichomfika ambapo akamjibu kwamba hapati kuswali, akamwambia:

“Hiki ni kitu ambacho Allaah amewaandikia wasichana wa Aadam.”

Ni wajibu kwa mwanamke aridhie mipango na makadirio ya Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kwamba hiki ni kitu ambacho Allaah amewaandikia wasichana wa Aadam kwa ajili ya kumliwaza. Kwa msemo mwingine ni kama anamwambia kwamba sio jambo maalum kwako. Kila msichana wa Aadam anajiwa na hedhi. Kwa hivyo nasema kwamba usitumie tembe hizi. Ukifunga ni kwa amri ya Allaah. Ukiacha kufunga ni kwa amri ya Allaah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (52) http://binothaimeen.net/content/1172
  • Imechapishwa: 05/07/2019