Ibn ´Uthaymiyn akiweka sawa maoni ya Ibn Taymiyyah juu ya swalah ya mkusanyiko

Swali: Je, kuna kitu kinachomlazimu mtu akiacha swalah ya mkusanyiko kwa kuchukulia wepesi pasi na udhuru?

Jibu: Mtu akiacha swalah ya mkusanyiko kwa kuchukulia wepesi pasi na udhuru kisha akaswali kivyake, hakika Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) anaona kuwa swalah yake ni batili. Kwa sababu yeye anaona kuwa mkusanyiko ni sharti juu ya kusihi kwa swalah. Kila mmoja anajua hadhi ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) inapokuja katika elimu, amana, dini na ufahamu. Maoni yake ni yenye nguvu. Lakini hata hivyo ni nyonge kwa upande fulani. Hivyo ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya mkusanyiko ni bora kuliko swalah ya anayeswali peke yake kwa daraja ishirini na saba.”

Hii ni dalili inayofahamisha kwamba swalah ya anayeswali peke yake ni sahihi. Vinginevyo isingelikuwa na ubora. Kwa hivyo maoni ya Shaykh-ul-Islaam katika jambo hili ni dhaifu.

Maoni ya sawa ni kwamba swalah ya mkusanyiko ni wajibu na sio sharti juu ya kusihi kwa swalah na kwamba yule ambaye ataacha kuswali na mkusanyiko anapata dhambi; amemuasi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ni mwenye kujifananisha na wanafiki ambao swalah ni mzigo kwao. Hali imefikia kiasi cha kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah nzito kwa wanafiki ni swalah ya ´Ishaa na swalah ya Fajr. Lau wangelijua yaliyomo ndani yake basi wangeziendea japo kwa kutambaa.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (66) http://binothaimeen.net/content/1503
  • Imechapishwa: 08/02/2020