Ibn Baaz nasaha kwa waislamu juu ya Ramadhaan


Swali: Ni maneno yepi ya maelekezo ambayo unawaelekezea Ummah wa Kiislamu kwa ajili ya mnasaba wa mwezi wa Ramadhaan?

Jibu: Mimi nawanasihi ndugu zangu waislamu walioko kila mahali kwa mnasaba wa kuingia mwezi wa Ramadhaan uliyobarikiwa wa mwaka 1413 juu ya kumcha Allaah (´Azza wa Jall), waikimbilie katika kheri, kuusiana kunako haki na kuwa na subira juu yake, kusaidiana juu ya wema na uchaji Allaah, kutahadhari na kila alichoharamisha Allaah katika maasi mbalimbali kila mahali na khaswa khaswa katika mwezi huu mtukufu. Kwa sababu ni mwezi mtukufu ambao matendo mema yanaongezwa ndani yake na madhambi kusamehewa kwa wale watakaofunga kwa imani na kwa matarajio. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[1]

”Inapoingia Ramadhaan basi milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa minyororo.”[2]

“Swawm ni kinga. Ikiwa ni mchana wa funga ya mmoja wenu basi asiseme maneno machafu na wala asifanye ujinga. Akiwepo mtu akamtukana basi aseme: “Mimi nimefunga.”[3]

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

كل عمل ابن آدم له، الحسنة بعشر أمثالها، إلا الصيام فإنه لي وأنا أجزي به، ترك شهوته وطعامه وشرابه من أجلي، للصائم فرحتان، فرحة عند فطره، وفرحة عند لقاء ربه، ولخلوف فم الصائم عند الله أطيب من ريح المسك

“Matendo yote ya mwanaadamu ni yake. Tendo jema mara kumi mfano wake. Isipokuwa tu swawm; hiyo ni Yangu na mimi ndiye Nitailipa. Ameacha matamanio yake, chakula chake na kinywaji chake kwa ajili yangu. Mfungaji ana furaha mbili; furaha wakati wa kukata swawm na furaha nyingine wakati wa kukutana na Mola wake. Furaha itokayo kinywani mwa mfungaji nzuri kuliko miski.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa bishara njema Maswahabah zake kwa kufika Ramadhaan na akiwaambia:

“Umekujieni mwezi wa Ramadhaan. Ni mwezi uliyobarikiwa. Allaah huteremsha ndani yake rehema, anafuta makosa, anaitikia du´aa na anajifakhari mbele ya Malaika wake. Muonyesheni Allaah kheri. Hakika mwangamivu ni yule atayenyimwa rehema za Allaah.”[5]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuutendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”[6]

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

Kuna Hadiyth nyingi ambazo zinaelezea fadhilah za mwezi wa Ramadhaan na zinazokokoteza juu ya kulipwa matendo maradufu.

Hivyo ninawausia ndugu zangu waislamu kunyooka katika michana yake na nyusiku zake na kushindana katika matendo yote ya kheri. Miongoni mwa hayo ni kusoma Qur-aan tukufu kwa wingi pamoja na mazingatio, kuielewa pamoja vilevile na kukithitisha kusema “Subhaan Allaah”, “Alhamdulillaah”, “Laa ilaaha ill Allaah”, “Allaahu Akbar”, “Astaghfir Allaah”, kumuomba Allaah Pepo, kumuomba akulinde na Moto na kuomba du´aa zengine zilizo nzuri.

Vilevile nawausia ndugu zangu kutoa swadaqah kwa wingi, kuwaunga mafukara na masikini, kutilia umuhimu kutoa zakaah kuwapa wape wenye kustahiki, kutilia umuhimu kulingania kwa Allaah, kumfunza mjinga, kuamrisha mema na kukataza maovu kwa upole, hekima na kwa kutumia njia nzuri pamoja vilevile na kujiepushe na madhambi yote na kushikamana na tawbah na kuwa na msimamo juu ya haki kwa kutendea kazi maneno Yake (Ta´ala):

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Tubuni kwa Allaah nyote, enyi waumini, mpate kufaulu.” (24:31)

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”Hakika wale waliosema: “Mola wetu ni Allaah” kisha wakanyooka, basi hakutokuwa na khofu juu yao na wala hawatohuzunika; hao ndio watu wa Pepo – ni wenye kudumu humo milele, ni malipo kwa yale waliyokuwa wakitenda.” (46:13 -14)

Ninamuomba Allaah awawafikishe wote katika yale anayoyapenda na kuyaridhia na awalinde wote kutokamana na fitina zenye kupotosha na mitego ya mashaytwaan.

[1] al-Bukhaariy (2014) na Muslim (760).

[2] al-Bukhaariy (1899) na Muslim (1079).

[3] al-Bukhaariy (1904).

[4] al-Bukhaariy (1904) na Muslim (1151).

[5] al-Bayhaqiy katika ”Majma´-uz-Zawaaid” (03/142).

[6] al-Bukhaariy (1903).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/48-50))
  • Imechapishwa: 16/05/2018