Ibn Baaz kwamba Salafiyyuun ndio kundi lililookoka

Swali: Makundi na mapote yanayosema kuwa ndio pote lililonusuriwa yamekuwa mengi na watu wengi yamewachanganya mambo haya. Tufanye nini na khaswa ukizingatia ya kwamba kuna makungi mengi yanayojinasibisha na Uislamu kama mfano wa Suufiyyah, Salafiyyah na mengineyo. Ni vipi tutapambanua?

Jibu: Imethibiti ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mayahudi wamefarikiana makundi 71.”

Bi maana wote wataingia Motoni isipokuwa moja tu ambao ni wale wafuasi wa Muusa (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam).

“Manaswara wamefarikiana makundi 72.”

Bi maana wote wataingia Motoni isipokuwa moja tu nao ni wale ambao waliomfuata ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam).

“Ummah huu pia utafarikiana makundi 73… “

Bi maana Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam).”

“Wote wataingia Motoni isipokuwa moja tu.”

Wakauliza ni lipi kundi litalookoka ambapo akasema:

“Ni mkusanyiko (al-Jamaa´ah).”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Ni wale watakaonifuata mimi na Maswahabah zangu.”

Hili ndio kundi lililookoka. Ni wale waliokusanyika juu ya haki aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakanyooka kwayo. Wameshikamana barabara na mfumo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Nao ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, Ahl-ul-Hadiyth na Salafiyyuun ambao wanawafuata wema waliotangulia na wakapita juu ya njia yao katika kutendea kazi Qur-aan na Sunnah. Makundi yote yanayokwenda tofauti na wao kuna khatari wakaingia Motoni.

Kwa ajili hiyo ndio maana unatakiwa kulitazama kila kundi linalosema kuwa ndio lililookoka. Yatazame matendo yao. Ikiwa matendo yao yanaafikiana na Shari´ah basi ndilo. Vinginevyo hapana. Inapokuja katika kila kundi mizani ni Qur-aan tukufu na Sunnah takasifu. Wale ambao matendo yao ni yenye kuafikiana na Qur-aan na Sunnah basi wanaingia ndani ya kundi lililookoka. Kuhusu yale makundi ambayo hali zao ni kinyume na hivo, kama mfano wa Jahmiyyah, Mu´tazilah, Raafidhwah, Murjii-ah na wengineo kama wale Suufiyyah waliopindukia ambao wanazua pasi na dalili kutoka kwa Allaah, wote wanaingia ndani ya yale makundi ambayo ameyatishia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba yataingia Motoni mpaka pale yatapotubia juu ya yale yanayokwenda kinyume na Shari´ah.

Kila kundi ambalo lina jambo linalokwenda kinyume na Shari´ah. Ni lazima kwao kutubia na kurejea katika haki aliyokuja nayo Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa njia hiyo ndio watasalimika kutokamana na matishio. Ama wakiendelea kubaki juu ya Bid´ah na wasifuate njia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi wanaingia ndani ya makundi yaliyotishiwa. Si kwamba wote ni makafiri. Wametishiwa tu kuingia Motoni. Kuna uwezekano katika wao kuna ambaye ni kafiri kwa sababu ya kufanya kitu katika kufuru. Kama ambavo kuna uwezekano akawepo ambaye si kafiri lakini hata hivyo ametishiwa kuingia Motoni kwa sababu ya Bid´ah zake katika dini na kuweka kwake Shari´ah katika dini kitu ambacho hakukiidhinisha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://binbaz.org.sa/mat/4723
  • Imechapishwa: 08/02/2019