Swali 05: Ni vipi watu watafunga ikitofautiana miezi miandamo? Je, ni lazima kwa wale walioko mbali kama Marekani na Australia kufunga na mwezi wa Saudi Arabia kwa kutouona mwezi?

Jibu: Maoni ya sawa ni kutegemea mwezi na kutozingatia kutofautiana kwa miandamo. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha kutegemea mwezi na hakupambanua katika jambo hilo. Hayo ni katika yale yaliyosihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Fungeni kwa kuuona [mwezi] na fungueni kwa kuuona mwezi. Mkifunikwa na mawingu basi kamilisheni idadi ya [siku] thelathini.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fungeni mpaka pale mtakapouona mwezi au mkamilishe idadi na wala msifungue mpaka pale mtakapouona mwezi au mkamilishe idadi.”

Kuna Hadiyth nyingi kuhusu maana hiyo. Hakuashiria (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kutofautiana kwa miezi miandamo ilihali ni mwenye kulijua jambo hilo.

Wapo wanachuoni wengine wenye kuona kwamba kila nchi ifuate mwezi mwandamo wao ikiwa miezi miandamo itatofautiana. Wametumia hoja kwa yale yaliyothibiti kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Hakutendea kazi mwezi wa watu wa Shaam na yeye alikuwa al-Madiynah (Radhiya Allaahu ´anh). Watu wa Shaam walikuwa wameona mwezi mwandamo usiku wa ijumaa na wakafunga kwa jambo hilo katika zama za Mu´aawiyah (Radhiya Allaahu ´anh).”

Kuhusu watu wa al-Madiynah hawakuuona isipokuwa usiku wa jumamosi. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alipoambiwa kuhusu uonekanaji wa mwezi wa watu wa Shaam na kwamba walifunga akasema:

“Sisi tuliuona usiku wa jumamosi. Tutaendelea kufunga mpaka tuuone tena au tukamilishe idadi.”

Akatumia hoja kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fungeni kwa kuuona [mwezi] na fungueni kwa kuuona mwezi. Mkifunikwa na mawingu basi kamilisheni idadi ya [siku] thelathini.”

Maoni haya yana nguvu fulani. Nimeona wanachama wa baraza la wanachuoni wakubwa Saudi Arabia wakishikamana nayo katika kuoanisha kati ya dalili.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdllaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah tata´alaqah bisw-Swiyaam, uk. 08-09
  • Imechapishwa: 05/04/2019