Himdi zote anastahiki Allaah pekee. Swalah na salamu zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake.

Amma ba´d:

Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote kuwa Israa´ na Mi´raaj ni katika alama kubwa za Allaah zenye kutolea dalili kufahamisha ukweli wa Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ukubwa wa manzilah yake mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Vilevile kuna dalili juu ya uwezo wa Allaah na kufahamisha kuwa yuko juu ya viumbe Wake wote (Subhaanah). Allaah (Ta´ala) amesema:

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha mja Wake usiku kutoka al-Masjid al-Haraam mpaka al-Masjid al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake [amechukuliwa] ili Tumuonyeshe baadhi ya alama Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote daima, Mwenye kuona yote daima.” (17:01)

Imepokelewa kwa njia mbalimbali kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alipandishwa mbinguni na akafunguliwa milango yake mpaka akapita mbingu ya saba. Mola Wake akamzungumzisha kwa yale aliyoyataka na akafaradhisha juu yake swalah tano. Mwanzoni (Subhaanah) alikuwa amemfaradhishia swalah khamsini. Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuacha kuwa ni mwenye kurejea Kwake na kumuomba uwepesishiwe mpaka akamfanyia zikawa tano. Ni faradhi tano lakini hata hivyo inapokuja katika thawabu ni khamsini; kwa sababu tendo jema moja linalipwa mara kumi – himdi na shukurani njema zote anastahiki Allaah.

Hakukuja katika Hadiyth Swahiyh yoyote yenye kusema kuwa Israa´ na Mi´raaj ilikuwa ni usiku fulani. Kila kilichokuja kulenga usiku maalum hakikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa mujibu wa wanachuoni wa Hadiyth. Allaah ni mwingi wa hekima kwa kuwasawazisha nayo watu. Lau hata kungelithibiti kuwa ni usiku maalum basi isingelijuzu kwa waislamu kukhusisha ndani yake kwa kufanya kitu chochote kile katika ´ibaadah na isingelijuzu kuusherehekea kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake hawakusherehekea na wala hawakufanya kitu maalum siku hiyo. Ikiwa kusherehekea ni kitu kimechowekwa katika Shari´ah basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angewabainishia Ummah kwa maneno au vitendo. Lau kungelipitika kitu katika hayo kingejulikana na kuwa wazi na hivyo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wangetunukulia. Kwani wametunukulia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yale yote ambayo Ummah unayahitajia na hawakupuuzia chochote kinachohusiana na dini. Maswahabah wao wametangulia katika kila kheri. Lau kusherehekea usiku huu ingelikuwa ni kitu kimechowekwa katika Shari´ah basi wao wangelikuwa ni wa kwanza kutangulia kukifanya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio mtu wa kwanza mwenye kuwatakia watu mema. Amefikisha ujumbe wake vile inavyostahiki na akatekeleza amana. Lau kuadhimisha usiku huu na kuusherehekea ingelikuwa ni sehemu katika dini ya Uislamu basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingeghafilika kwacho na asingeweza kuficha hilo. Ilipokuwa hakukupitika kitu katika hayo, basi ikajulikana kuwa kuusherehekea na kuuadhimisha ni kitu kisichokuwa na uhusiano wowote ule na Uislamu. Allaah ameukamilishia Ummah huu dini na kuutimizia neema na akamkemea yule mwenye kuweka Shari´ah katika dini yale ambayo hakuyaidhinisha. Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (05:03)

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةُ الْفَصْلِ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea kwayo idhini? Na lau si neno la uamuzi [ulokwishapita], bila shaka ingelikidhiwa baina yao; na hakika madhalimu watapata adhabu iumizayo.” (42:21)

Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ambazo ni Swahiyh akitahadharisha Bid´ah na kuweka wazi kuwa ni upotevu kwa lengo la kuwazindua Ummah kuwaonesha ukhatari wake na kuwaogopesha kuyavumbua. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayezusha katika dini yetu hii yasiyokuwemo basi atarudishiwa mwenyewe.”

Katika upokezi wa Muslim imekuja:

“Mwenye kufanya kitendo ambacho hamna ndani yake dini yetu atarudishiwa mwenyewe.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika Khutbah zake siku ya Ijumaa:

“Amma ba´d: Hakika maneno bora kabisa ni Kitabu cha Allaah, uongofu bora kabisa ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mambo maovu kabisa ni ya kuzua, hakika kila Bid´ah ni upotevu.”

Katika Sunan kumepokelewa kupitia kwa al-´Arbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutolea mawaidha makali ambayo yalitikisa mioyo yetu na macho yetu yakatiririka machozi. Tukasema: “Ee Mtume wa Allaah! Kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga, basi tuusie.” Ndipo akasema: “Ninakuusieni usikivu na utiifu hata kama mtatawaliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo bara bara na mziume kwa magego. Tahadharini na mambo ya kuzua! Hakika kila kitakachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

Hadiyth zenye maana kama hii ni nyingi.

Imethibiti kutoka kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Salaf-us-Swaalih wakitahadharisha juu ya Bid´ah. Si kwa jengine isipokuwa ni kwa sababu ni nyongeza katika dini na Shari´ah ambayo Allaah hakuiidhinisha. Huko ni kujifananisha na maadui wa Allaah miongoni mwa mayahudi na manaswara ambao wameongeza katika dini zao na kufuata yale ambayo Allaah hakuyapa idhini. Hilo linalazimisha kuutukana Uislamu na kuutuhumu kutokamilika. Ni jambo lenye kujulikana kuwa kufanya hivi ni ufisadi mkubwa na maovu yenye kutia aibu. Isitoshe ni kupingana na maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu.” (05:03)

Vilevile ni kwenda kinyume wazi wazi na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo zinatahadharisha Bid´ah na kuwakimbiza watu kwazo.

Tunataraji zile dalili tulizotaja ndani yake mna kutosheleza na ukinaishaji kwa yule mwenye kutaka haki juu ya kutahadharisha Bid´ah hizi na kusherehekea usiku wa Israa´ na Mi´raaj na kutahadharisha nayo na kwamba ni kitu kisichokuwa na uhusiano wowote kabisa na Uislamu.

Pale ambapo Allaah aliwajibisha kutoa nasaha kwa waislamu, kuwabainishia yale aliyoyawekea Shari´ah katika dini na akaharamisha kuficha elimu ndipo nikaonelea kuwazindua ndugu zangu juu ya Bid´ah hii ambayo imeenea katika miji mingi mpaka ikafia kiasi cha kwamba baadhi ya watu wakafikiria kuwa ni katika dini. Allaah ndiye mwenye jukumu la kuzitengeneza hali za waislamu wote na kuwatunuku uelewa katika dini na kutuwafikisha sisi na wao kushikamana na haki na kuwa na uthabati juu yake na wakati huo huo kuachana na yale yenye kwenda kinyume nayo. Hakika Yeye ndiye mwenye kusimamia na muweza wa hilo.

Swalah na salamu zimwendee mja na Mtume Wake Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (03/45-46)
  • Imechapishwa: 28/08/2020