Swali: Nimesikia fatwa yako kwenye moja katika kanda zako ukijuzisha kuoa katika nchi za ugenini na wakati huohuo mwanamume akanuia kumwacha baada ya muda fulani pindi tu kutapomalizika kongamano au masomo. Ni ipi tofauti kati ya ndoa hii na ndoa ya Mut´ah? Inakuweje pale ambapo mke wake anapozaa mtoto? Je, amwache katika nchi za ugenini na mama yake mtalikiwa? Naomba kuwekewa wazi.

Jibu: Ni kweli kwamba al-Lajnah ad-Daaimah, na mimi ndiye raisi wake, imetoa fatwa juu ya kufaa kuoa kwa nia ya talaka ikiwa nia hiyo iko kati ya mja na Mola Wake. Akioa katika nchi ya ugenini na nia yake ni kwamba pindi atapomaliza masomo yake, kazi yake na mfano wa hayo atamwacha mwanamke huyo[1], wanachuoni wengi wanaona kuwa hakuna ubaya kufanya hivo. Nia hii inakuwa baina yake yeye na Allaah (Subhaanah). Si kwamba ni sharti.

Tofauti kati yake na Mut´ah ni kwamba ndoa ya Mut´ah kunakuwa na sharti kwa kipindi maalum kwa mfano mwezi, miezi miwili, mwaka mmoja, miaka miwili na kadhalika. Ukimalizika muda uliopangwa basi ndoa inafutika. Hii ndio ndoa ya Mut´ah ambayo ni batili. Lakini kitendo cha yeye kumuoa kwa mujibu wa Sunnah ya Allaah na Mtume Wake lakini ndani ya moyo wake akanuia kwamba pindi atapomaliza shida zake nchini atamwacha ni kitu kisichomdhuru. Isitoshe nia hii inaweza kubadilika, haitambuliki na si kwamba ni sharti. Bali ni kitu kilichoko kati yake yeye na Allaah. Jengine ni kwamba kufanya hivo ni miongoni mwa sababu zinazomlinda na uzinzi na machafu. Haya ndio maoni ya wanachuoni wengi. Ameyanukuu mtunzi wa “al-Mughniy” ambaye ni Muwaffaq-ud-Diyn Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) kutoka kwao.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/kuoa-kwa-nia-ya-talaka-ni-kumhadaa-mwanamke

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/26) https://binbaz.org.sa/fatwas/154/%D8%A7%D9%84%D9%86%D9%83%D8%A7%D8%AD-%D8%A8%D9%86%D9%8A%D8%A9-%D8%A7%D9%84%D8%B7%D9%84%D8%A7%D9%82
  • Imechapishwa: 27/12/2019