Ibn Baaz kukusanyika nyumbani kwa maiti kwa ajili ya Khitmah

Swali: Kumsomea Qur-aan maiti kwa njia ya kuweka misahafu nyumbani kwa maiti ambapo wakaja baadhi ya majirani na wale waliokuwa wakimtambua maiti na kila mmoja kwa mfano akamsomea juzu moja. Baada ya hapo watu wakarudi makazini kwao na asipewe yeyote pesa yoyote. Baada ya kumaliza kumsomea maiti wakamwombea du´aa maiti na wakaomba thawabu za kisomo cha Qur-aan kumwendea maiti. Je, kisomo na du´aa hii inamfikia maiti na analipwa kwayo?

Jibu: Kitendo hichi na mfano wake hakina msingi. Hakukuhifadhiwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) kwamba walikuwa wakiwasomea maiti. Bali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake na al-Bukhaariy akaiwekea taaliki katika “as-Swahiyh” yake kwa njia ya kukata.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema katika Khutbah yake ya ijumaa:

“Amma ba´d: Hakika mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

an-Nasaa´iy ameongeza kwa cheni ya wapokezi Swahiyh:

“Na kila upotevu ni Motoni.”

Kuhusu kuwatolea swadaqah maiti na kuwaombea du´aa ni mambo yanayowafaa na yanawafikia kwa maafikiano ya waislamu.

[1] Muslim (867) kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiy Allaahu ´anhumaa).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/339) https://binbaz.org.sa/fatwas/kind/1?page=11
  • Imechapishwa: 25/01/2020