Swali: Tumejua kupitia barnamiji hii ya kwamba haipiti Talaka kwa mwenye hedhi na mwenye mimba. Je, ni kuwa haipiti kabisa au inapita baada ya Twahara?

Jibu: Talaka ya mwenye hedhi haipiti kutokana na kauli sahihi (yenye nguvu) ya wanachuoni, tofauti na kauli ya jamhuri. Jamhuri ya wanachuoni wanaona kuwa inapita. Hali kadhalika kwa mwenye nifasi. Lakini kauli ya sahihi katika kauli za wanachuoni, na ndio waliokuwa wakifutu baadhi ya Taabi´iyn na Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) na akaichagua Shayk-ul-Islaam bin Taymiyyah, mwanafunzi wake Ibn al-Qayyim na kundi katika wanachuoni, kuwa Talaka hii haipiti. Kwa kuwa inakwenda kinyume na Shari´ah ya Allaah, kwa kuwa Allaah Kawekea Shari´ah kumtaliki mwanamke katika hali ya Twahara ya nifasi, hedhi na katika Twahara ambayo mume wake hakumjamii. Hii ndio Talaka ya Kishari´ah. Akimtaliki katika hedhi, nifasi au Twahara ambayo amemjamii, Talaka hii ni Bid´ah na wala haipiti kutokana na kauli ya sahihi ya wanachuoni. Kwa Kauli ya Allaah (Jalla wa ´Alaa):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ

“Ee Nabii! Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda (twahara na si katika hedhi) zao.” (65:01)

Bi maana katika Twahara ya jimaa. Namna hii ndivyo walivyosema wanachuoni kuhusu (maana ya) “watalikini katika wakati wa eda.” Wawe Twahara hawakuingiliwa au wawe na ujauzito. Hii ndio Talaka ya katika eda. Ama Talaka ya mjamzito wanachuoni wanaona kuwa inapita, na mwenye kusema kuwa haipiti kakosea. Talaka ya mjamzito inapita kwa wanachuoni, Talaka isiyopita ni ya mwenye hedhi na nifasi na Twahara ambayo mwanamke kaingiliwa na hakujadhihiri mimba yake. Talaka hizi (sampuli tatu) hazipiti kutokana na kauli ya sahihi ya wanachuoni, kwa kuwa zinakhalifu na Shari´ah ya Allaah na vile vile ni katika hali ambayo haikuwekwa Talaka kama tulivyotangulia kusema. Na baadhi ya ´Awwaam wanastaajabu na kusema Talaka ya mjamzito haipiti, hili ni kosa. Hii ni katika kauli za ´Awwaam zisizokuwa na asli katika Shari´ah wala maneno ya wanachuoni. Mjamzito Talaka inapita. Ni wajibu kujua hilo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb
  • Imechapishwa: 01/04/2018