Ibn Baaz kuhusu swalah ya tawbah na kuwa na dhana mbaya baada ya kutubia

Swali: Nilikuwa bado kijana nilifanya baadhi ya maasi. Nilitubu kwa Allaah lakini bado katika nafsi yangu nahizi kitu. Nimesikia kuhusu swalah ya tawbah. Naomba unipe faida juu ya hili.

Jibu: Tawbah inafuta yaliyo kabla yake na himdi zote zinamstahikia Allaah. Haitakikani kubaki kwenye moyo wako kitu katika hayo. Lililo la wajibu ni wewe kumjengea dhana nzuri Mola wako na uamini kuwa Allaah amekusamehe maadamu ulikuwa mkweli katika kutubu kwako. Kwa kuwa Allaah amesema:

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Tubuni kwa Allaah nyote, enyi waumini, mpate kufaulu.”[1]

Amefungamanisha kufaulu kwa tawbah. Mwenye kutubu basi amefaulu. Amesema (Subhaanah):

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

“Hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akaendelea kuongoka.”[2]

Hakika Yeye (Subhaanah) ni mkweli katika maelezo na ahadi Yake. Amesema (Subhaanah):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ

“Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya kwelikweli, huenda Mola wenu akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni kwenye mabustani yapitayo chini yake mito.”[3]

Neno “huenda” kwa Allaah inakuwa ni wajibu.

Ni wajibu kwako kumjengea dhana nzuri Mola wako. Unatakiwa uwe mkweli katika tawbah yako, mwenye kujutia ulichokifanya, mwenye kujivua nacho na mwenye kunuia kutokirudi. Nakutahadharisha kutokamana na wasiwasi. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema katika Hadiyth ya kiungu:

أنا عند ظن عبدي بي

“Mimi niko vile mja wangu anavyonidhania.”

Kwa hivyo unatakiwa kumdhania Allaah vyema. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Asife mmoja wenu isipokuwa awe anamdhania Allaah vyema.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Kuhusu swalah ya tawbah imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia kwa as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesema:

“Hakuna mja atayetenda dhambi kisha akajitwaharisha na akaifanya vizuri twahara halafu akaswali Rak´ah mbili kisha akamuomba Allaah msamaha kwa dhambi yake isipokuwa Allaah humsamehe.”

[1] 24:31

[2] 20:82

[3] 66:08

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/227-228)
  • Imechapishwa: 02/07/2017