Ibn Baaz kuhusu kusherehekea maulidi

Himdi zote anastahiki Allaah Pekee. Swalah na salamu zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake, Maswahabah zake na wenye kufuata uongofu wake.

Amma ba´d:

Kumekuja maswali mengi yenye kukariri yanayouliza juu ya hukumu ya kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuyasimamia, kumtolea Salaam na mengineyo yanayofanywa katika Maulidi.

Jibu ni kama ifuatavyo: haijuzu kushereheka mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala ya mwingine. Kwa sababu hiyo ni katika Bid´ah iliyozuliwa katika dini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuyafanya, makhaliyfah wake waongofu, mtu mwengine katika Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wala Taabi´uun yeyote katika karne bora. Watu hawa ni wajuzi zaidi juu ya Sunnah na wana mapenzi kamilifu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wenye kufuata Shari´ah yake zaidi kuliko waliokuja baada yao. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Mwenye kuzua katika dini yetu hii yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth nyingine:

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu baada yangu. Shikamaneni nazo na mziume kwa magego. Tahadharini na mambo ya kuzua! Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

Katika Hadiyth hizi mbili kuna maonyo makali juu ya kuzua Bid´ah na kuitendea kazi. Allaah (Subhaanah) amesema katika Kitabu Chake chenye kubainisha:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

“Na lolote lile analokupeni Mtume, basi lichukueni, na lolote lile analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah.” (59:07)

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitina au ikawasibu adhabu iumizayo.” (24:63)

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Kwa hakika mna kigezo kizuri kwa Mtume wa Allaah kwa mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamdhukuru Allaah kwa wingi.” (33:21)

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Na wale waliotangulia awali miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema Allaah Ameridhika nao nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito. Ni wenye kudumu humo milele – huko ndiko kufuzu kukuu.” (09:100)

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (05:03)

Aayah zilizo na maana kama hii ni nyingi.

Kuzusha mazao kama haya kinachopata kufahamika ndani yake ni kuwa Allaah (Subhaanah) hakuukamilishia Ummah huu dini na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufikisha yale ambayo Ummah wanatakiwa kuyatendea kazi mpaka walipokuja hawa waliokuja nyuma na wakawa wamezua katika Shari´ah ya Allaah yale ambayo hakuyatolea dalili. Wamefanya hivyo na huku wanadai kuwa wayafanyayo yanawakurubisha kwa Allaah. Hili, bila ya shaka, ndani yake kuna khatari kubwa na ni kupingana na Allaah (Subhaanah) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Allaah (Subhaanah) amewakamilishia waja Wake dini na akawatimizia neema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefikisha ufikisho wa wazi. Hakuacha njia inamyofikisha mtu Peponi na kumuweka mtu mbali na Moto isipokuwa amewabainishia nayo Ummah. Imethibiti katika Hadiyth Swahiyh kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hakutuma Mtume yeyote isipokuwa ilikuwa ni haki juu yake awaelekeze Ummah wake katika kheri anayoijua kwao na awatahadharishe na shari anayoijua kwao.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Ni jambo linalojulikana kuwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio Mtume bora kabisa, wa mwisho wao, mfikishaji na mnasihiaji mkamilifu zaidi. Lau kusherehekea Maulidi ingelikuwa ni sehemu katika dini ambayo Allaah (Subhaanah) anairidhia basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliwabainishia Ummah au angalau kwa uchache angelipatapo kuyafanya katika maisha yake au Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) wangeliyafanya. Pale ambapo hakukupatikana kitu katika hayo ndipo ikapata kujulikana kuwa Maulidi hayana lolote kuhusiana na Uislamu. Bali ni katika mambo yaliyozuliwa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameutahadharisha Ummah wake nayo, jambo ambalo tumetangulia kulisema katika Hadiyth mbili zilizotangulia. Kuna Hadiyth zingine zimekuja zikiwa na maana kama hiyo. Baadhi yazo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Khutbah ya Ijumaa:

“Amma ba´d: Hakika maneno bora kabisa ni Kitabu cha Allaah, uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), uovu wa mambo ni ya kuzua, hakika kila Bid´ah ni upotevu.”

Ameipokea Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Aayah na Hadiyth juu ya mada hii ni nyingi.

Kuna wanachuoni ambao wameweka wazi kuyakemea Maulidi na kutahadharisha juu yake kwa kutendea kazi dalili zilizotajwa na nyinginezo wakati baadhi ya wengine waliokuja nyuma wakaenda kinyume na kuyajuzisha. Kwa sharti yakiwa hayana maovu yoyote. Maovu hayo ni kama kuvuka mipaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanawake kuchanganyika na wanaume, kutumia ala za muziki na mengineyo ambayo yanapingwa na Shari´ah hii twaharifu. Wanachuoni hao walifikiria kuwa ni miongoni mwa Bid´ah zilizo nzuri. Kanuni ya Kishari´ah inasema kurudisha yale ambayo watu wametofautiana kwayo katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni [njia] bora na matokeo mazuri zaidi.” (04:59)

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ

“Na katika jambo lolote lile mlilokhitilafiana ndani yake, basi hukumu yake ni kwa Allaah.” (42:10)

Tumeyarudisha masuala haya – ambayo ni kusherehekea mazazi ya Mtume – katika Qur-aan. Tumechopata kuona ni kwamba inatuamrisha kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale aliyokuja nayo na inatuonya na yale aliyokataza. Qur-aan inatukhabarisha kuwa Allaah (Subhaanah) ameukamilishia Ummah huu dini. Sherehe hii sio miongoni mwa yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo hayana nafasi katika dini ambayo Allaah ametukamilishia nayo na kutuamrisha kumfuata Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika dini hiyo.

Hali kadhalika tumeyarudisha katika Sunnah na hatukupata kuona kuwa aliyafanya, kuyaamrisha wala Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) kuyafanya. Hayo yakatufahamisha kuwa sio katika dini. Bali kinyume chake ni katika Bid´ah iliyozushwa. Vilevile isitoshe ni kujifananisha na mayahudi na manaswara katika sherehe zao.

Kwa hayo inapata kujulikana kwa kila ambaye ana ujuzi angalau kidogo na malengo yake ni haki na uadilifu katika kutafuta kwake ya kwamba kusherehekea Maulidi sio katika dini ya Uislamu. Kinyume chake ni katika Bid´ah zilizozuliwa ambazo Allaah (Subhaanah) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wameamrisha kuyaacha na kutahadharisha nayo.

Haitakikani kwa mwenye busara kudanganyika na watu wengi wenye kuyafanya katika miji mbali mbali. Haki haijulikani kwa wengi wa wenye kuifanya. Haki inajulikana kupitia dalili za Kishari´ah. Allaah (Ta´ala) amesema juu ya mayahudi na manaswara:

وَقَالُوا لَن يَدْخُلَ الْجَنَّةَ إِلَّا مَن كَانَ هُودًا أَوْ نَصَارَىٰ ۗ تِلْكَ أَمَانِيُّهُمْ ۗ قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Na walisema: “Hatoingia Peponi isipokuwa aliyekuwa myahudi au mnaswara.” Hilo ni tamanio lao. Sema: “Leteni ushahidi wenu wa wazi mkiwa ni wakweli”.” (02:111)

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ

“Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah.” (06:116)

Isitoshe jengine ni kuwa sherehe hizi za Maulidi, pamoja na kuwa ni Bid´ah, mara nyingi ndani yake hakukosi maovu. Baadhi ya maovu hayo ni kama wanawake kuchanganyika na wanaume, muziki na nyimbo, pombe na madawa ya kulevya na maovu mengineyo. Sivyo tu, bali kunaweza kutokea kubwa kuliko hayo. Nacho ni shirki kubwa kwa njia ya kuvuka mipaka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au walii mwingine kwa kumuomba, kumtaka msaada na uokozi, kuamini kuwa anajua elimu ya mambo yaliyofichikana na mengineyo katika mambo ya kikafiri ambayo yanafanya watu wengi wakati wanaposherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ya wengine miongoni mwa wale wanaowaita kuwa ni “mawalii”. Imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Tahadharini na kupetuka mipaka katika dini. Hakika kilichowaangamiza waliokuwa kabla yenu ilikuwa ni kuvuka mipaka katika dini.”

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msinisifu kupindukia kama walivyofanya manaswara kwa mwana wa Maryam. Hakika mimi ni mja. Hivyo semeni “mja wa Allaah na Mtume Wake.”

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh).

Miongoni mwa maajabu ni kuwa watu wengi ni wachangamfu na ni wenye bidii kuhudhuria sherehe hizi zilizozuliwa na kuzitetea na wanakwepa yale ambayo Allaah ameyawajibisha juu yao katika kuhudhuria Ijumaa na swalah za mkusanyiko na kwao wanaona si lolote si chochote. Sambamba na hilo hawaoni kuwa wanafanya maovu makubwa. Bila shaka hilo ni kutokamana na udhaifu wa imani na uchache wa elimu na madoa mengi yaliyoko kwenye nyoyo miongoni mwa aina mbali mbali ya madhambi na maasi. Tunamuomba Allaah atupe afya sisi na waislamu wengine.

Miongoni mwa maovu hayo ni kuwa baadhi ya watu wanadhania kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anahudhuria Maulidi. Hii ni batili ilio kubwa kabisa na ujinga mbaya sana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatoki kwenye kaburi lake kabla ya siku ya Qiyaamah, hana mawasiliano na mtu yeyote na hahudhurii mikusanyiko yao. Bali atabaki kuwemo ndani ya kaburi lake mpaka siku ya Qiyaamah na roho yake iko katika starehe kubwa kabisa kwa Mola Wake Peponi. Amesema (Ta´ala) katika Suurah “al-Mu´muniyn”:

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ

“Kisha hakika nyinyi siku ya Qiyaamah mtafufuliwa.” (23:15)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi ndio mtu wa kwanza ambaye nitatoka ndani ya kaburi siku ya Qiyaamah, mimi ndio muombezi wa kwanza na ndiye wa kwanza atayepewa uombezi.”

Aayah na Hadiyth hii na nyenginezo zenye maana kama hii zote zinafahamisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maiti wengine watatoka ndani ya makaburi yao siku ya Qiyaamah. Hili ni jambo ambalo wanachuoni wa waislamu wamekubaliana juu yake na hawakutofautiana juu yake.

Inapaswa kwa waislamu kuzinduka kwa mambo haya na kutahadhari na yale yaliyozuliwa na wajinga na Bid´ah na ukhurafi mwingine wenye kufanana na hayo ambayo Allaah hakuteremsha dalili yoyote juu yake.

Kuhusiana na kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni miongoni mwa ´ibaadah bora kabisa na matendo mema. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Hakika Allaah na Malaika wake wanamswalia Mtume. Enyi mlioamini mswalieni na msalimieni maamkizi ya amani.” (33:56)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuniswalia mara moja basi Allaah atamswalia mara kumi.”

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kufanya hivo katika nyakati zote na limekokotezwa zaidi mwisho wa kila swalah. Bali ni jambo la wajibu kwa wanachuoni wote katika Tashahhud ya mwisho katika kila swalah na ni Sunnah iliyokokotezwa mahali pengi. Miongoni mwa sehemu hiyo ni baada ya adhaana, wakati anapotajwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), siku ya Ijumaa na usiku wa kumkia Ijumaa, kama zilivyofahamisha hilo Hadiyth nyingi.

Allaah ndiye mwenye jukumu la kutuwafikisha sisi na waislamu wengine wote katika kuweza kuielewa dini, kuwa imara juu yake na kututunukia kushikamana na Sunnah na kutahadhari na Bid´ah. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, ahli zake na Maswahabah zake wote.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (3/10-12)
  • Imechapishwa: 22/08/2020