Ibn Baaz kuhusu kusema mtu fulani yuko Peponi au Motoni

Swali: Ni ipi hukumu ya ambaye anamkatia muislamu ya kwamba atakuwa miongoni mwa watu wa Motoni pamoja na kuzingatia ya kwamba anajisalimisha na mafunzo ya Kiislamu?

Jibu: Haijuzu kumshuhudilia yeyote si Pepo wala Moto isipokuwa tu yule aliyeshuhudiliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Asiseme ya kwamba yuko Pepo wala Motoni. Haijalishi kitu hata kama mtu ni katika wachaji haitakiwi kusema kuwa ni katika watu wa Peponi. Haijalishi kitu hata kama mtu ni katika watenda maasi haitakiwi kusema kuwa ni katika watu wa Motoni. Bali hata kama atakuwa mshirikina/kafiri. Haitakiwi kusema kuwa ni katika watu wa Motoni. Anaweza kutubia. Badala yake inatakiwa kusema endapo atakufa juu ya shirki basi ni katika watu wa Motoni na endapo atakufa juu ya imani ni katika watu wa Peponi. Ama kusema fulani mwana wa fulani katika watu wa Peponi au kusema fulani mwana wa fulani ni katika watu wa Motoni haifai. Muumini na muislamu wanaweza kuritadi na wanaweza kubadilika kama ambavyo vilevile kafiri anaweza kuingia katika Uislamu. Kwa ajili hii Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameafikiana ya kwamba haifai kumshuhudilia yeyote Pepo wala Moto isipokuwa tu yule aliyeshuhudiliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au dalili za Qur-aan zikafahamisha hivo. Kama mfano wa Abu Lahab. Qur-aan imefahamisha kuwa ni katika watu wa Motoni. Huyu anashuhudiliwa kuwa ni katika watu wa Motoni:

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ

“Imeteketea mikono miwili ya Abu Lahab na ameteketea.” (111:01)

Hali kadhalika ambaye amekufa katika ukafiri na ikatambulika kuwa amekufa katika kufuru anatakiwa kushuhudiliwa kuwa ni katika watu wa Motoni. Kama mfano wa Abu Jahl, Abu Twaalib, ´Utbah bin Rabiy´ah na Shu´bah bin Rabiy´ah. Watu hawa waliuawa siku ya Badr katika ukafiri. Hivyo ikatambulika kuwa ni katika watu wa Motoni.

Vilevile wanatakiwa kushuhudiliwa Pepo wale walioshuhudiliwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kama mfano wa wale makhaliyfah watatu ambao wameshuhudiliwa Pepo. Wale Maswahabah kumi wengine waliobaki ambao wameshuhudiliwa Pepo ambao ni ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Twalhah bin ´Ubaydillaah, az-Zubayr bin al-´Awaam, Sa´d bin Abiy Waqqaas, Abu ´Ubaydah bin al-Jarraah na Sa´iyd bin Zayd bin ´Amr bin Nufayl. Hawa ndio wale tisa waliobaki wataoingia Peponi. Vivyo hivyo inahusiana pia na Thaabit bin Qays bin Shammaas, ´Ukkaashah bin Muhswin. Hawa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye kawashuhudilia Pepo. Vilevile ´Abdullaah bin Salaam.

Tunachotaka kusema ni kuwa yule ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemshuhudia Pepo ni katika watu wa Peponi. Lakini badala yake tunatakiwa kusema kuwa waumini wote wako Peponi. Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wote wako Peponi. Lakini hatumkatii yeyote kwa dhati yake ya kwamba fulani mwana wa fulani yuko Peponi isipokuwa yule aliyekatiwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vilevile tunatakiwa kusema kwa ujumla ya kwamba makafiri wakifa katika kufuru ni katika watu wa Motoni.  Hatusema ya kwamba fulani mwana wa fulani amekufa katika ukafiri. Kwa sababu hatujui. Lakini akifa katika ukafiri basi ni katika watu wa Motoni.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.binbaz.org.sa/noor/8805
  • Imechapishwa: 25/07/2017