Ibn Baaz Kuhusu Allaah Alimuumba Aadam Kwa Sura Yake II

Swali: Imethibiti katika Hadiyth ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikataza kuukebehi uso na kwamba Allaah amemuumba Aadam kwa sura Yake. Ni ipi imani sahihi kuhusu Hadiyth hii?

Jibu: Hadiyth imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo amesema:

“Atapopiga mmoja wenu basi aepuke uso. Hakika Allaah amemuumba Aadam kwa sura Yake.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… kwa sura ya ar-Rahmaan.”

Hili halipelekei kushabihisha na kulifananisha. Maana yake kwa mujibu wa wanachuoni ni kwamba Allaah amemuumba Aadam hali ya kuwa ni mwenye kusikia, mwenye kuona na mwenye kuzungumza kile anachotaka. Huu ndio wasifu wa Allaah pia (´Azza wa Jall). Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote, Mwenye kuzungumza na Mwenye uso (Jalla wa ´Alaa). Haina maana ya kushabihisha na kufananisha. Sura ya Allaah sio kama sura walizonazo viumbe. Maana yake ni kwamba ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote, Aliye na uso na Anazungumza pale anapotaka. Kadhalika amemuumba Aadam hali ya kuwa ni mwenye kusikia, mwenye kuona, mwenye uso, mwenye mkono, aliye na unyayo na anazungumza anapotaka. Lakini hata hivyo kusikia kwa Aadam sio kama kusikia kwa Allaah, kuona kwa Aadam sio kama kuona kwa Allaah, kuzungumza kwa Aadam sio kama kuzungumza kwa Allaah na uso wa Aadam sio kama uso wa Allaah. Allaah (Subhaanah) ana sifa zinazolingana Naye na kiumbe ana sifa zinazolingana naye. Sifa za viumbe zina kuisha, kasoro na mapungufu. Kuhusu sifa za Allaah ni kamilifu na haziingiliwi na upungufu, udhaifu wowote, kuisha wala kuondoka. Kwa ajili hii ndio maana amesema (´Azza wa Jall):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

”Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.”(112:04)

Kwa hivyo haijuzu kwa mtu kupiga uso wala kuukebehi uso.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.binbaz.org.sa/noor/11483
  • Imechapishwa: 28/01/2017