Ibn ´Abdil-Wahhaab hukumu ya anayewatukana Maswahabah

Kumepokelewa mapokezi mengi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayofahamisha ukamilifu wa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na khaswa wale makhaliyfah waongofu. Hakika yaliyotajwa katika kumsifu kila mmoja yanatambulika na bali yamepokelewa kwa njia tele. Walionakili hayo ni watu wengi ambao ni muhali wakaafikiana juu ya uongo. Mkusanyiko wa maelezo yao yanapelekea katika elimu yenye yakini juu ya ukamilifu wa Maswahabah na ubora wa makhaliyfah.

Ukishatambua kuwa Aayah za Qur-aan zimekuja nyingi zikielezea ubora wao na vivyo hivyo Hadiyth zilizopokelewa kwa njia nyingi zinafahamisha ukamilifu wao, hivyo basi yule mwenye kuamini ufasiki wao au kwamba wengi wao ndio mafasiki na kwamba wameritadi au kwamba wengi wao ndio wameritadi kutoka katika dini au akaonelea ni sawa kuwatukana na kwamba hilo linaruhusu au akawatukana na wakati huohuo akaonelea kuwa ni haki na ni halali kufanya hivo, amemkufuru Allaah (Ta´ala) na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale waliyoelezea juu ya ubora wao na ukamilifu wao unaolazimisha kuwa mbali na yale yanayopelekea katika ufasiki, kuritadi na haki au kujuzu kutukanywa. Yule atakayemkadhibisha Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika yale yaliyothibiti kutoka kwao amekufuru pia. Mtu kutojua yaliyopokelewa kwa njia tele (Mutawaatir) kwa hali ya kukata kabisa sio udhuru. Haisaidii kitu vilevile kuyafasiri kimakosa kinyume na dalili yenye kuzingatiwa. Ni kama mfano wa kupinga kwamba vipindi vitano vya swalah sio faradhi, kwa ujinga huyu anakuwa kafiri. Vivyo hivyo inahusiana na kama ataipindisha kwa maana tusiyoijua, amekufuru. Elimu za Qur-aan na Hadiyth zinazofahamisha juu ya uboro wake ni zenye kukata kabisa.

Yule mwenye kuwatukana baadhi yao, ikiwa ni miongoni mwa wale kumepokelewa nukuu nyingi juu ya ubora na ukamilifu wao, kama makhaliyfah, na akaonelea ni haki au imeruhusiwa kuwatukana, amekufuru kwa kukadhibisha yale yaliyothibiti kabisa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwenye kumkadhibisha ni kafiri. Endapo atamtukana pasi na kuamini kuwa ni haki au imeruhusiwa kufanya hivo, basi ametenda dhambi nzito. Kwa kuwa kumtukana muislamu ni dhambi nzito.

Kuna wanachuoni ambao wameonelea kuwa mwenye kumtukana Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ni kafiri kabisa – Allaah ndiye anajua zaidi.

Ikiwa ni yule ambaye hayakupokelewa mapokezi mengi juu ya ubora na ukamilifu wake, udhahiri ni kwamba kumtukana kwake itakuwa ni dhambi nzito. Isipokuwa tu ikiwa kama atamtukana kwa ajili ya kusuhubiana kwake na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika hali hiyo itakuwa ni ukafiri.

Raafidhwah wengi wanaowatukana Maswahabah na khaswa khaswa wale makhaliyfah wanaonelea kuwa ni haki au imeruhusiwa kuwatukana. Kuna ambao wanaonelea kuwa ni wajibu kufanya hivo. Kwa kuwa wanajikurubisha kwa kufanya hivo kwa Allaah (Ta´ala). Wanaona hilo ni katika mambo matukufu zaidi katika dini yao. Hayo yamenakiliwa kutoka kwao. Ni upotevu wa akili uliyoje wa watu wanaojikurubisha kwa Allaah (Ta´ala) kwa mambo yanayopelekea kukhasirika kwa dini yao! Allaah ndiye Mwenye kuhifadhi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaa ar-Raafidhwah, uk. 59-64
  • Imechapishwa: 29/04/2017