Huyu amewazidi hata Khawaarij


Swali: Kuna baadhi ya watu huenda wakamkufurisha mtu kwa sababu ndogo tu au kwa dhambi yoyote ile.

Jibu: Mtu huyu ambaye anawakufurisha watu kwa sababu au dhambi yoyote – ikiwa taabiri hii ni kweli “kwa dhambi yoyote ile” – madhehebu yake yanakuwa mabaya zaidi kuliko ya Khawaarij. Madhehebu ya Khawaarij wanamkufurisha mwenye kutenda dhambi kubwa na si dhambi zote. Akipatikana leo mwenye kuwakufurisha waislamu kwa dhambi yoyote ile, basi ni mpotevu mwenye kwenda kinyume na Qur-aan na Sunnah na amezidisha juu ya madhehebu ya Khawaarij ambao ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) aliwapiga vita na waislamu wakatofautiana juu ya kuwakufurisha kwao; kuna walioonelea hivyo na wengine wakaonelea kuwa ni watenda madhambi makubwa na wakawafanya kuwa ni katika waasi na madhalimu. Si  Allaah ndiye amesema:

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا

“Endapo mtajiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa, basi Tutakufutieni madhambi yenu madogo na tutakuingizeni katika mahali patukufu.”?[1]

Mtu kwa kujiepusha na madhambi makubwa Allaah anamsamehe madhambi madogo. Hapa ni pale ambapo hatoendelea katika madhambi hayo madogo. Ama akiendelea juu yake, wanachuoni wamesema:

“Kuendelea juu ya madhambi madogo kunayafanya makubwa.”

Hakuna shaka juu ya kwamba msemo huu ni upotevu. Isitoshe aliyesema hivi atambue kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kumwita ndugu yake “ee kafiri” na hali hayuko hivo, basi inamrejelea yeye mwenyewe.”

Yeye ndiye anakuwa kafiri. Haya yamesemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Endapo hatokuwa kafiri duniani basi atakuwa kafiri mbele ya Allaah. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema ni lazima mmoja wao awe ndio kafiri.

[1] 04:31

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa' ash-Shahriy (15)
  • Imechapishwa: 13/12/2017