Hukumu ya wanawake kusagana katika Uislamu

Mwanamke ni kama mwanamume ameamrishwa kuyateremsha macho yake na kuhifadhi tupu yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ

“Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao. Hivyo ni utakaso zaidi kwao. Hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale wayatendayo. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao.”[1]

Shaykh wetu Muhammad al-Aamiyn ash-Shanqiytwiy (Rahimahu Allaah) amesema katika Tafsiyr yake “Adhwaa´-ul-Bayaan”:

“Allaah (Jalla wa ´Alaa) amewaamrisha waumini wa kiume na wa kike kuteremsha macho na wahifadhi tupu zao. Katika kuhifadhi tupu kunaingia vilevile kujihifadhi kutokamana na uzinzi, liwati, mambo ya kusagana, kudhihirisha kwa watu na kujionyesha kwao.” Mpaka aliposema: “Allaah (Ta´ala) amewaahidi wale wenye kutekeleza maamrisho Yake katika Aayah hii katika wanaume na wanawake msamaha na ujira mkubwa wakifanya zile sifa zilizotajwa katika Suurah ya “al-Ahzaab” isemayo:

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ

“Hakika waislamu wanaume na wanawake… “[2]

Mpaka aliposema:

وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

“… wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake, basi Allaah amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.”[3]

Maneno yake “Mambo ya kusagana” ni mwanamke kumwendea mwanamke mwenzake kwa kusagana. Hiyo ni dhambi kubwa ambayo watendaji hao wawili wanastahiki kutiwa adabu zitazowakomesha kwelikweli.

Mtunzi wa “al-Mughniy”[4] amesema:

“Wanawake wawili wakisagana basi hao ni wazinifu wawili waliolaaniwa kutokana na yale yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Mwanamke akimwendea mwanamke mwenzake basi hao ni wazinifu.”

Ni lazima kuwaadhibu kwa sababu ni uzinzi usiokuwa na kikomo.”[5]

Kwa hiyo mwanamke wa Kiislamu – na khaswakhaswa wasichana – anatakiwa kutahadhari kutokamana na kitendo hichi kichafu.

[1] 24:30-31

[2] 33:35

[3] 33:35 (06/186-187).

[4] Uk. (08/198).

[5] Yamesemwa na Shaykh-ul-Islaam katika ”Majmuu´-ul-Fataawaa” (15/321). Kujengea juu ya haya mwanamke msagaji anaitwa mzinifu, kama ilivyokuja katika Hadiyth:

”Zinaa ya wanawake ni kusagana kwao.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat ´alaa Ahkaam Takhtasswu bil-Mu´minaat, uk. 119-120
  • Imechapishwa: 20/10/2019