Swali: Kuna mtu anaumwa figo na anaona kuwa ana uwezo wa kulipa madeni yake ya Ramadhaan. Lakini wiki nzima hawezi kufunga isipokuwa tu siku moja, nayo ni siku ya ijumaa. Hiyo ndio siku pekee ambayo hafanyi kazi. Siku ya alkhamisi hufua na siku nyenginezo zilizobaki anafundisha. Hawezi kufunga isipokuwa tu siku ya ijumaa. Je, anaweza kufunga siku ya ijumaa pekee au asubiri mpaka atapokuwa na likizo ya majira ya joto ndio afunge?

Jibu: Mimi naona kuwa asubiri mpaka atapokuwa na likizo ya majira ya joto. Muda ni mpana wa kufunga madeni ya Ramadhaan. Mtu anaweza kuchelewesha mpaka pale kutapobaki katika Sha´baan kiwango cha yale masiku ya kufunga anayodaiwa.

Kuhusu kufunga siku ya ijumaa kunajuzu ikiwa kimetokana na sababu. Ikiwa hakuna sababu iliyopelekea basi imechukizwa mtu kuifunga peke yake. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwa mmoja katika wakeze ilihali amefunga siku ya ijumaa ambapo akamuuliza: “Jana ulifunga?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Utafunga kesho?” Akasema: “Hapana.” Akamwambia: “Basi fungua.” Akamwamrisha afungue ili asiipwekeshe siku ya ijumaa.

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikataza kukhusisha siku ya ijumaa kufunga au usiku wa kuamkia ijumaa kwa kusimama usiku kwa ajili ya swalah.

Lau tukikadiria kuwa mtu amehitajia kufunga siku hiyo, au amefunga siku ya ijumaa si kwa sababu ni siku ya ijumaa, lakini ni kwa sababu imekumbana na siku ya ´Arafah, siku ya ´Aashuuraa´. Katika hali hiyo hakuna neno kwake. Kwa sababu hakufunga siku ya ijumaa kwa sababu ni ijumaa. Bali amefunga kwa sababu ni siku ya ´Arafah, siku ya ´Aashuuraa´ na mfano wa hayo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (42) http://binothaimeen.net/content/91
  • Imechapishwa: 04/05/2018