Hukumu ya kuchelewesha Fajr mpaka wakati wa kwenda kazini


Swali: Ni ipi hukumu kwa yule ambaye mara nyingi haamki kuswali Fajr isipokuwa pale anapoamka kwa ajili ya kwenda kazini takriban saa moja na nusu pamoja na kuzingatia kwamba hachelewi kazini kwake kwa dakika hata moja. Kwa sababu anapupia arekodiwe kuwa miongoni mwa wale wenye kuja mapema kazini.

Jibu: Baadhi ya wanachuoni wanaona kuwa mwenye kuacha swalah moja tu mpaka wakati wake ukatoka pasi na udhuru kwamba ni kafiri ukafiri mkubwa wenye kumtoa katika Uislamu. Kujengea juu ya hili mtu huyu anakuwa ni kafiri mwenye ukafiri wenye kumtoa katika Uislamu. Kwa sababu kuchelewesha swalah mpaka baada ya wakati kwa makusudi pasi na udhuru wa Kishari´ah iwapo ataiswali haitosaidia kitu na wala haitokubaliwa kutoka kwake.

Wengine wanaona kuwa kuacha swalah ambako kumemaanishwa kuwa ni ukafiri ni kule mtu akaacha kabisa; hana cha swalah ya Fajr wala nyenginezo. Maoni haya ndio yako karibu zaidi na usawa kwa mujibu wa udhahiri wa maandiko. Mtu huyu hakufuru kujengea juu ya maoni haya ambayo tunayapa nguvu. Lakini hata hivyo yuko kwenye khatari kubwa. Hapa ni pale ambapo haoni kuwa inafaa kuchelewesha Fajr mpaka baada ya kuingia wakati wake. Katika hali hiyo atahesabika kuwa amepinga ufaradhi wake na hivyo anakufuru kwa kupinga.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (72) http://binothaimeen.net/content/1662
  • Imechapishwa: 11/04/2020