Hukumu ya kubadilisha nia katikati ya swalah

Swali: Ni ipi hukumu ya kubadilisha nia katikati ya swalah? Kwa mfano nimesahau kuwa sijaswali Dhuhr ambapo ikafika swalah ya ´Aswr, nikaingia kuswali ´Aswr kwa kunuia ´Aswr, nilipofika katika Rak´ah ya tatu nikakumbuka kuwa sijaswali Dhuhr ambapo nikabadilisha nia. Ni kipi kinachonilazimu?

Jibu: Alipobadilisha nia kutoka katika ´Aswr kwenda katika Dhuhr ameibatilisha ´Aswr au hakuibatilisha? Ameibatilisha. Kwa hiyo ´Aswr imebatilika. Aliponuia Dhuhr nia yake imesihi ilihali hakunuia tokea mwanzoni mwake? Kwa hiyo swalah mbili zote zimebatilika. Kwa hiyo ni wajibu kwake kuirudi Dhuhr na ´Aswr. Mfano wa hali kama hii endapo mtu analazimika kuswali Dhuhr na akaingia kuswali ´Aswr kwa kusahau ambapo akaja kukumbuka katikati ya swalah, tunamwambia aendelee na swalah yake kwa kujengea ya kwamba anaswali ´Aswr. Atapomaliza ndio aswali Dhuhr. Katika hali hii unasamehewa suala la kupangilia kwa sababu umesahau. Allaah (Ta´ala) amesema:

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[1]

Lakini ukiwa umeshaingia ndani ya swalah ya Sunnah kisha ukakumbuka kuwa hujaswali swalah ya faradhi, ikate swalah ya sunnah na uingie katika ile swalah ya faradhi kuanzia mwanzo wake.

[1] 02:286

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (45) http://binothaimeen.net/content/1048
  • Imechapishwa: 17/07/2020