Hongereni wafungaji


Ndugu! Sisi tuko katika mwezi wa Ramadhaan uliobarikiwa ambao ndio bwana wa miezi na ambao Allaah ameuteua kuteremsha Qur-aan ndani yake. Ameuteua funga ndani yake iwe ni moja katika nguzo tano za Uislamu ambayo Uislamu hauwezi kusimama na kunyooka isipokuwa kwayo. Hongera kwa yule ambaye atamtakasia nia yake kwa Allaah. Hongera kwa yule atakayefunga hali ya kumtakasia nia Allaah na akafunga kwa kuamini, kutaraji, kupenda na kutaka mwenyewe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebashiri ya kwamba inafuta madhambi. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mwenye kufunga Ramadhaan kwa imani na kwa matarajio basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Hii ni bishara njema kwa kila muislamu aliyefunga midhali atatekeleza masharti haya; akafunga kwa kuamini Allaah na Mtume wake, uwekwaji wake katika Shari´ah, kuamini thawabu zake, kwa kunuia, kupenda na kutaka mwenyewe. Asifunge kwa sababu ya kujionyesha, kufuata kibubusa wala kuwafuata watu wengine. Mfungaji anapaswa kujiepusha na madhambi makubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Swalah vipindi vitano, ijumaa moja hadi nyingine na Ramadhaan moja hadi nyingine ni vyenye kufuta yaliyo baina yake midhali mtu ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa.”

Allaah anasamehe makosa ya mtu midhali ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa. Madhambi makubwa ni yale yenye kupelekea mtu akaadhibiwa hapahapa duniani au akatishiwa matishio makali huko Aakhirah kama mfano wa kutiwa Motoni, kulaaniwa, kughadhibikiwa au akavuliwa imani kama vile wizi, uzinzi, unywaji pombe, kuwaasi wazazi wawili, kuwakata ndugu zako, kula ribaa, rushwa, usengenyi, kuenea uvumi, kushambulia damu za watu, mali za watu, kuvunja heshima za watu, kutumia vibaya haki za watu, kuuza bidhaa kwa viapo vya uongo, kuficha kasoro za bidhaa na mengineyo. Ni lazima kwa mtu akaacha madhambi makubwa kama haya.

Miongoni mwa madhambi makubwa pia ni kuchelewesha swalah mpaka ukatoka wakati wake. Kwa mfano mtu akachelewesha swalah ya Fajr na akaiswali baada ya jua kuchomoza. Akachelewesha Dhuhr na akaikusanya pamoja na ´Aswr. Akaswali ´Aswr pale jua linapokaribia kuzama. Matendo haya ni katika madhambi makubwa. Allaah anafuta makosa ya mtu maadamu atakuwa ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa na pindi atapokuwa ni mwenye kumwamini Allaah na Mtume wake. Kwa msemo mwingine amefunga kwa kuamini na kutaraji na kunuia thawabu.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://shrajhi.com.sa/uploads/9%20%D8%A3%D8%B9%D9%85%D8%A7%D9%84%20%D8%A7%D9%84%D8%AE%D9%8A%D8%B1%20%D9%81%D9%8A%20%D8%B1%D9%85%D8%B6%D8%A7%D9%86.mp3
  • Imechapishwa: 15/05/2019