Swali: Wanazuoni wengi wanasema kuwa mtawala anayehukumu kinyume na Shari´ah ikiwa haonelei kuwa ni halali kufanya hivo na anatambua kuwa hukumu ya Allaah ndio bora zaidi basi hawi kafiri. Ni ipi dalili inayoonyesha kwamba hakufuru isipokuwa mpaka awe mwenye kuhalalisha jambo hilo? Ni vipi tutajua kuwa anaonelea kuwa ni halali kwa sababu ni jambo linahusiana na moyo?

Jibu: Mosi ni lazima tujue kwamba kumkufurisha mtu maana yake ni kumtoa nje ya Uislamu na kumwingiza ndani ya ukafiri. Hili linapelekea katika hukumu kubwa. Moja wapi ni kuhalalisha kuuliwa na kuchukua mali yake. Hili ni jambo kubwa. Haijuzu kwetu kulichukulia wepesi. Kwa mfano kusema kitu fulani ni halali na kitu fulani ni haramu pasi na elimu ni jepesi kuliko kusema mtu fulani ni kafiri na muislamu pasi na elimu.

Takfiyr na Uislamu ni kazi ya Allaah. Tukiziangalia dalili, basi tutaona namna ambavo Allaah amewasifu wale wanaohukumu kinyume na yale aliyoteremsha Allaah kwa njia tatu:

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri.” ( 05:44)

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio madhalimu.” (05:45)

وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Yeyote asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio mafasiki.” (05:47)

Pia amesema kuwa kuhukumu kinyume na Shari´ah kwamba ni “ujinga” na akasema:

أَفَحُكْمَ الْجَاهِلِيَّةِ يَبْغُونَ ۚ وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ

“Je, wanataka hukumu za kipindi cha kijahili? Na nani mbora zaidi kuliko Allaah katika kuhukumu kwa watu wenye yakini.” (05:50)

Kwa hivyo ni lazima kuwepo ufumbuzi wa sifa hizi ambazo zinaonekana kama vile kupingana. Hakuna ufumbuzi mwingine zaidi ya kuzifanyia kazi kwa misingi ya ki-Shari´ah.

Akija mtu akafuta hukumu ya Shari´ah na akaweka badala yake hukumu za binadamu zinazopingana na yale Allaah aliyomteremshia Mtume Wake, hapana shaka yoyote kwamba mtu huyu ni mwenye kuhalalisha. Kwa sababu amefuta Shari´ah kikamilifu na akaweka badala yake hukumu kutoka kichwani mwake au hukumu kutoka kwa mwengine ambayo ni mbaya zaidi kuliko yake. Huyu ni kafiri.

Wakati anapofuta hukumu ya Shari´ah na kuweka badala yake hukumu za binadamu, hiyo ina maana kwamba amehalalisha jambo hilo. Lakini je, mtu huyu anakufurishwa? Au mtu asubiri mpaka pale hoja itakapomsimamia? Kuna uwezekano anachanganya mambo ya kidunia kwa mambo yanayohusiana na ´Aqiydah na ´ibaadah. Kwa ajili hiyo utamuona namna anavyoiheshimu ´ibaadah na wala haibadilishi. Hasemi kwa mfano watu wacheleweshe swalah ya Dhuhr mpaka  ´Aswr kwa sababu watu wako makazini wakati wa adhuhuri au watu waswali ´Ishaa wakati wa Maghrib kwa sababu watu wanataka kulala mapema. Anaheshimu jambo hili. Lakini inapokuja katika mambo ya kidunia, pengine akawa na ujasira wa kuja na hukumu za binadamu zinazopingana na dini. Hapana shaka yoyote kwamba ni ukafiri kwa vile anafuta hukumu ya Shari´ah na akaweka badala yake kitu kingine.

Lakini hata hivyo ni lazima kumsimamishia hoja. Ni lazima tumuulize ni kwa nini amefanya hivo. Pengine amedanganywa na baadhi ya wanazuoni. Wako wanazuoni wanaofanya kazi kwa ajili ya nchi na wanazikengeusha dalili kwa ajili ya kutaka kumridhisha mtawala. Kwa mfano wanasema kuwa mambo ya kidunia kama vile ya kiuchumi, ya kilimo na ya kupokea na kuchukua ni kazi ya mwanadamu kwa sababu manufaa yake yanatofautiana. Kisha wanambabaisha kwa maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika nyinyi ni wajuzi zaidi juu ya mambo ya dunia yenu.”

Watawala wengi wa hivi sasa ni wajinga. Hawajui chochote. Anapokuja mtu anayeonekana kwa uinje kuwa na elimu na akasema kuwa suala fulani linatokana na manufaa na manufaa yanatofautiana kutegemea na zama, maeneo na hali na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema “Hakika nyinyi ni wajuzi zaidi juu ya mambo ya dunia yenu” na hapana ubaya wowote kutumia hukumu za binadamu zilizokuwa zimefichikana wakati wa Maswahabah na zinazoendana na hali ya sasa na matokeo yake wakahalalisha yale aliyoharamisha Allaah. Kwa mfano wanasema kuwa kuna aina mbili za ribaa; ribaa zinazohusiana na mabenki na ribaa zinazohusiana na watu masikini na kwamba hiyo aina ya kwanza inafaa na aina ya pili ndio haramu. Kisha baada ya hapo akatia saini. Ni mjinga.

Lakini tukimbainishia hoja na kumwambia kwamba ni kosa na upotoshaji kutoka kwa mwanachuoni huyu ambaye amekudanganya na wakati huohuo akaendelea juu ya yale anayofanya, basi hapo ndipo tutamhukumu kwamba ni kafiri.

Kwa msemo mwingine ni kwamba wanazuoni wamefanya mgawanyo huu ili dalili hizi ambazo hazikufungamanishwa ziweze kuoana na misingi ya kidini na inayotambulika.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (87 A)
  • Imechapishwa: 16/06/2021