Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake [wote] wa waumini – ya kwamba [nje ya nyumbani] wajiteremshie jilbaab zao; hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane [kuwa ni wanawake wa heshima] na wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[1]

Haya ndio yaliyoamrishwa na Allaah na Mtume wake kuwaamrisha wanawake wa waumini. Kisha baada ya hayo anakuja mtu anayeitwa Muhammad Salaamah katika Tweet yake na anamkosoa kila yule anayelingania wanawake kujisitiri hali ya kuwa ni mwenye kusifu kitendo hicho kwamba ni jambo la kipuuzi na utovu wa adabu. Amesema:

“Wanawake ni kama wanaume.”

Pia amesema:

“Miongoni mwa mambo ya ajabu ni kwamba mimi nazungumzia qadhiya hii na sisi tuko katika mwaka wa 2018.”

Pia amesema:

“Uislamu haukuamrisha Hijaab kwa njia kama hii ya kiyahudi na ya ki-Orthodox. Si vyenginevyo isipokuwa ni desturi na mila ambazo ni lazima kuzitokomeza na kuzimaliza.”

Namna hii ndivo alivyosema hali ya kuwa ni mwenye kutupilia mbali yale yaliyotajwa katika Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya waislamu. Namna hii ndivo ujinga na kujifanya mjinga kunavowafanya watu wake!

Wanawake kuvaa Hijaab ni maamrisho ya Kishari´ah yaliyothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu wakeze Mtume ambao ndio viigizo vya wanawake wa waislamu:

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

“Mnapowauliza basi waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.”[2]

´Aaishah, ambaye ni mama wa waumini (Radhiya Allaahu ´anhaa), amesema:

“Wapanda farasi wanaume walikuwa wakitupitia na sisi tuko kwenye Ihraam pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanapotukaribia, kila mmoja wetu anateremsha mavazi yake ya juu, Jilbaab, usoni mwake. Wanapokuwa wameshapita, tunajifunua tena.”

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameeleza kuwa mwanamke kuvaa Hijaab kunazisafisha mioyo ya wanaume na wanawake, kunawazuia wanaume waovu kuwaudhi wanawake na kunamjaza heshima mwanamke. Sambamba na hilo mwanamke kujiacha waziwazi ni njia inayopelekea kumwondoshea heshima na wanaume waovu kumshambulia. Hayo yanashuhudiwa katika jamii ambazo wanawake hawajisitiri mbele ya wanaume.

Sifa nzote njema anastahiki Allaah kuona waislamu ni wenye kushikamana barabara na yale yaliyokuja katika Kitabu cha Mola wao na Sunnah za Mtume wao katika adabu za wanawake na wanapuuzilia mbali sauti hizi zenye kutisha zinazoongea maneno kama haya. Allaah (Ta´ala) ni Mwenye kuinusuru dini Yake, Kitabu Chake na Sunnah za Mtume wake japokuwa watachukia wale wenye kuchukia:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi Tumeteremsha Ukumbusho na hakika Sisi bila shaka ndio Tutakaoihifadhi.”[3]

Himdi zote anastahiki Allaah. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] 33:59

[2] 33:53

[3] 15:09

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.alfawzan.af.org.sa/ar/node/17650
  • Imechapishwa: 03/04/2019