Haya ndio unayotakiwa kuzingatia kwa anayekuja kumposa msichana wako

Swali: Nataraji utaniwekea wazi mstahiki. Kwani mstahiki mbele za watu anatofautiana katika uelewa wao. Kwa sababu wako watu ambao wanaweza kuwakatalia watu kwa sababu hatoki katika nchi yake, hawana hadhi moja au wana mali ndogo kuliko. Tunaomba utuwekee wazi hilo Allaah akuwafikishe.

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha mstahiki kwa njia ya wazi pale aliposema:

“Atapokujieni yule ambaye mnaridhia kwake dini na tabia yake basi muozesheni.”

Mwanamke wa Thaabit bin Qays bin Shammaas (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamwambia:

“Ee Mtume wa Allaah! Thaabit bin Qays simtii dosari katika tabia wala dini.”

Hii ni dalili inayoonyesha kwamba kitu kikubwa kinachozingatiwa ni tabia na dini.

Kuhusu yale yaliyoenea kwa watu hii leo kwamba hamuozeshi mtu kwa sababu hatokamani na kabila lake, hamuozeshi yeyote isipokuwa kutoka katika watoto wa ndugu zake au kwa mfano anasema kumwambia kwamba wako kabila tofauti, yote haya ni makosa na hayana msingi. Bali mtu anatakiwia kumuozesha mtu asiyekuwa katika kabila lake. Mbora mbele ya Allaah ni yule ambaye ni mchaji Allaah zaidi. Hizi ni katika chembechembe ambazo kamwe mtu hatakiwi kuzizingatia. Kinachozingatiwa ni tabia na dini. Hivi hamjui kuwa Hadiyth nyingi ambazo tumenukuliwa zimenukuliwa na wale ambao sio waarabu na wakaipa kipaumbele dini ya Uislamu? Ni wingi wa wanachuoni walioje ambao sio waarabu? Kwa ajili hii nataraji kwamba watu hawatozingatia isipokuwa mambo mawili peke yake; tabia na dini.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (45) http://binothaimeen.net/content/1060
  • Imechapishwa: 19/03/2019