Haya ndio huwafanya wengi kutumbukia katika maasi

Swali: Mimi ni kijana mwenye msimamo na hutumbukia kwenye dhambi siku zote. Kila ninapotubu hutumbukia kwenye dhambi hiyo. Nimeona haya kuendelea kuomba tawbah kisha narudi kuifanya dhambi hiyo. Unaninasihi nini?

Jibu: Ninakunasihi kutubu kila pale unapotumbukia kwenye dhambi. Fanya hivo hata kama litakariri. Usikate tama na rehema za Allaah. Usione haya kwa Allaah na ukaacha kufanya tawbah. Tubu kwa Allaah! Allaah amekuamrisha utubu:

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ

“Wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi basi humdhukuru Allaah wakaomba msamaha kwa madhambi yao.” (03:135)

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚإِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا

“Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka katika [kujidhulumu] nafsi zao msikate tamaa na rehema ya Allaah, hakika Allaah anasamehe madhambi yote.” (39:53)

Tubu kila pale utapofanya dhambi na usikate tamaa ya kukubaliwa au ukasema kuwa unaona haya kwa Allaah. Ikiwa kweli unaona haya basi tubu kwa Allaah (´Azza wa Jall). Haijalishi kitu hata kama utakariri kufanya hivo.

Lakini jiepushe na sababu zinazokufanya kurudi katika maasi. Huenda una marafiki waovu na wanakusababishia kutumbukia kwenye madhambi, unakaa na watu waovu n.k. Jiepusha na kukaa na watu waovu. Ikiwa unaangalia vitu vichafu vinavyopelekea katika fitina, kama mfano wa picha mbaya, chaneli za ngono n.k., jiepushe na sababu zinazokufanya kutumbukia kwenye maasi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tafsiyr al-Mufasswal (58) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/tf–1432-01-14.mp3
  • Imechapishwa: 21/08/2020