Swali: Je, kutoka katika maandamano na kufanya mapinduzi na kuwalea vijana juu yake ni katika mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni mamoja hayo yanafanywa ndani ya miji ya Kiislamu au nje yake? Ni ipi nasaha yako kwa mwenye kufanya huo ni mfumo wa kulingania?

Jibu: Huo ni mfumo wa Marx, Lenin na mfano wao. Sio mfumo wa Kiislamu. Mapinduzi, kumwaga damu, fitina na matatizo ni mfumo wa Marx na Lenin ukiongeza juu yake vilevile mfumo Khawaarij na wakaita kuwa ni “Uislamu”. Kama kawaida yao wanaita “muziki wa Kiislamu”, “ujamaa wa Kiislamu”, “demokrasia ya Kiislamu” na “katiba ya Kiislamu”. Kila aina ya upotevu na majanga wanaotoa mashariki na magharibi wanayavisha vazi la Kiislamu. Allaah ameutakasa Uislamu kutokamana na njia hizi. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.” (16:125)

Jihaad ina milango na masharti yake. Haihusiani na njia hizi za wa kina Marx ambazo wanazivisha vazi la Kiislamu. Wamechukua mapinduzi na ujamaa huu kutoka kwa kina Marx na Lenin. Demokrasia wameichukua kutoka Amerika. Halafu wanajifanya kuwa wanaipiga vita Marekani ilihali upande mwingine wanaeneza fikira za kimarekani. Ninaapa kwa Allaah ya kwamba wanazieneza. Kuwepo kwa makundi makundi, ugatuzi wa madaraka, upigaji kura na maandamano yote haya ni fikira za kimarekani. Fikira hizo zinatolewa mamiliyari ya mapesa kwa ajili ya kuzisambaza ulimwenguni. Watu hawa ndio wahuduma wakubwa wa Marekani na wenye kuzisambaza fikira hizi. Halafu pamoja na yote haya wanawatuhumu watu wengine kuwa ni vibaraka vya Marekani.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 17
  • Imechapishwa: 04/11/2016