Swali 13: Vipi kuhusu ambaye anakataza watu kumuombea du´aa mtawala?

Jibu: Kitendo hichi ni kutokana na ujinga wake na kutokuwa na elimu. Kwa sababu kumuombea du´aa mtawala ni miongoni mwa mambo makubwa ya mtu kujikurubisha kwa Allaah, miongoni mwa utiifu ulio mkubwa na ni miongoni mwa kutoa nasaha kwa ajili ya Allaah na waja Wake. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoambiwa: “Hakika [kabila la] Daws wameasi na ni makafiri.” Akasema:

“Ee Allaah! Waongoze Daws na uwalete.”[1]

Matokeo yake Allaah akawaongoza na akawaleta hali ya kuwa ni waislamu. Muumini ni yule mwenye kuwaombea watu kheri. Mtawala ana haki zaidi ya kuombewa du´aa. Kwa sababu kuongoka kwake ni kuongoka kwa Ummah. Kumuombea du´aa ni miongoni mwa du´aa na nasaha muhimu zaidi. Anatakiwa kuombewa awafikishwe kuiendea haki, asaidiwe kwayo, Allaah amjaalie marafiki wazuri na Allaah amtosheleze kutokamana na shari za nafsi zake na shari za marafiki waovu. Kwa hivyo kumuombea du´aa ya kuafikishwa, uongofu, kuongozwa kwa moyo, matendo na marafiki wazuri ni miongoni mwa mambo muhimu sana na mambo bora ya mtu kujikurubisha kwayo kwa Allaah. Imepokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ya kwamba amesema:

“Lau ningelijua mimi kwamba nina du´aa yenye kuitikiwa basi ningeijaalia kwa mtawala.”

Hayo pia yamepokelewa kutoka kwa al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Rahimahu Allaah).

[1] al-Bukhaariy (2937) na Muslim (2524).

  • Mhusika: Imaam ´Abdu-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa ´Ulamaa-ul-Kibaar fiy al-Irhaab wat-Tadmiyr, uk. 113-114
  • Imechapishwa: 28/02/2020