Hataki kuzaa sana kwa ajili ya kupata muda wa ´ibaadah   

Swali: Kuna mwanaume ana watoto wane na anasema kuwa anataka kusitisha kizazi na atosheke na watoto alionao ili apate muda wa kutosha wa kumuabudu Mola Wake kwa sababu kuzaa watoto wengi kunasumbua. Je, anapata dhambi kwa kufanya hivo au hapana?

Jibu: Mtazamo huu ni mpungufu. Kuwalea watoto ni katika kumtii Allaah. Watoto wakiongoka kupitia mikono yako watakunufaisha sawa katika hali ya uhai na ukishakufa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapokufa mtu matendo yake pia hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah yenye kuendelea, elimu yenye kunufaika kwayo au mtoto mwema mwenye kumuombea.”

Jengine tunamwambia ni kwamba: kuwa na watoto wengi ni kuuongeza Ummah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amehimiza mtu aoe mwanamke mwenye mapenzi na mwenye kuzaa sana ili azae watoto wengi na akaeleza kuwa atajifakhari kwao mbele ya Mitume wenzake siku ya Qiyaamah. Muulizaji aachane na mwelekeo huu na azae watoto wengi ili riziki yake iweze kuongezeka, waongoke kupitia mikono yake na sababu nyingine ili watoto wamnufaishe katika uhai wake na baada ya kufa kwake. Vilevile kama tulivyosema ili kuhakikisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aweze kujifakhari siku ya Qiyaamah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (07)
  • Imechapishwa: 01/05/2020