Hapa ndipo swalah ya ijumaa itawalazimu wafanya kazi

Swali: Baadhi ya wafanya kazi wamenieleza kuwa mabosi wao hawawaachi kwenda kuswali swalah ya ijumaa kwa sababu wanafanya kazi kama walinzi wa mashamba. Wamenitaka kuwaulizia swali hili na kuwahamasisha waajiri kuwaacha waende kuswali swalah ya ijumaa. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Ikiwa wafanya kazi wako mbali kabisa na msikiti kiasi cha kwamba hawawezi kusikia adhaana bila kipaza sauti na isitoshe wako nje ya mji, basi swalah ya ijumaa haiwalazimu. Wahakikishiwe kuwa si wenye kupata dhambi kwa kule kubaki kwao shambani na badala yake waswali Dhuhr huko. Pamoja na hivyo ashaariwe mwajiri wao kwamba awape idhini. Hilo ni bora kwake na kwao pia wakenda kuswali swalah ya ijumaa. Isitoshe pengine hilo likawa ni sababu ya kuwapa uchangamfu wa kufanya kazi vizuri tofauti kama wanafanyiwa dhiki sana. Wafanya kazi wengi wanataka kuja kuswali ijumaa ili waweze kukutana na marafiki na jamaa zao. Kwa ajili hiyo utawaona wanakuja kuswali ijumaa na kuketi sokoni mpaka pale imamu anapokuja. Anapokuja imamu ndipo wanaingia msikitini na wanaendelea kuzungumza ndani ya msikiti na huku imamu anatoa Khutbah. Kitendo kama hichi kinajulisha kuwa mtu hakulenga kuja kuswali swalah ya ijumaa. Alichotaka ni kutangamana na marafiki na jamaa zake – na Allaah ndiye mjuzi zaidi wa nia.

Kwa hali yoyote, kama wanasikia adhaana pasi na kipaza sauti na wanaishi ndani ya mji, basi wanatakiwa kwenda katika swalah ya ijumaa. Kama wanaishi nje ya mji basi hakuna kinachowalazimu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (14 A)
  • Imechapishwa: 29/01/2021