Swali: Inakuweje kuwachukia watu wa Bid´ah kwa ajili ya Allaah ambao iwapo tutawahama basi jambo hilo litapelekea katika madhara makubwa kuliko ikiwa tutaenda kinyume na kuwanasihi?

Jibu: Kukata ni suluhu na dawa ambayo mtu anaitumia pale inapokuwa ni yenye kusaidia na inaachwa pale inapokuwa haisaidii. Mzushi na mtenda maasi hadharani wanastahiki kukatwa baada ya kunasihiwa, kuelekezwa katika kheri, kuamrishwa kumtii Allaah na kuwakataza yale aliyokataza, kubainishiwa kosa na Bid´ah yake. Akiendelea na asikubali nasaha basi anastahiki kukatwa.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwakata watatu katika Maswahabah bora pindi walipobaki nyuma katika vita vya Tabuuk pasi na udhuru. Miongoni mwao ilikuwa ni pamoja na Ka´b bin Maalik. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waislamu wengine waliwasusa nyusiku khamsini. Baadaye Allaah akawakubalia tawbah yao na hivyo wakaacha kuwakata na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waislamu wakaanza kuwatolea salamu. Allaah aliteremsha juu yao maneno Yake (Ta´ala):

لَّقَد تَّابَ اللَّـهُ عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika Allaah amepokea tawbah ya Nabii na Muhajiruun na Answaar ambao wamemfuata katika saa ya dhiki baada ya nyoyo za kundi miongoni mwao zilikaribia kupondoka kisha akapokea tawbah yao. Hakika Yeye kwao ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[1]

Akasema baada yake:

وَعَلَى الثَّلَاثَةِ الَّذِينَ خُلِّفُوا

“Na ya wale watatu waliobaki nyuma… “[2]

Lengo ni kwamba kususa ni suluhu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waislamu wengine wakawasusa hawa watatu kwa sababu kulikuwa na manufaa katika jambo hilo. Lengo pia ili wengine wapate kuogopa kubaki nyuma vitani na katika mapambano wakati kunapoamrishwa jambo hilo.

Kimaanishwacho ni kwamba mtu anatakiwa kutazama manufaa wakati wa kukata. Ikiwa manufaa yanapelekea kukata na kujitenga mbali na mtu, basi mtu atafanya hivo kwani pengine akatubu na kujutia. Na ikiwa manufaa hayapelekei kuendelea na nasaha na kukumbusha, basi mtu atafanya hivo. Haya yanajulikana na kila mtu kwa kuzingatia.

Mtenda maasi au mzushi huyo akiwa yeye ndiye kiongozi, mfalme, raisi wa nchi, raisi wa kabila na mkuu wa kabila na jambo la kumkata linapelekea katika madhara makubwa, basi ni lazima katika hali hiyo kumfanyia upole, kumlingania kwa Allaah na kumnasihi daima ili maovu yake yasizidi na asiwadhuru Ummah. Vivyo hivyo kuhusu ambaye anaonyesha wazi maasi yake. Hukumu hii ni juu ya wazushi na watenda maasi waziwazi.

[1] 09:117

[2] 09:118

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4137/%D9%85%D8%A7-%D8%A7%D9%84%D8%AD%D9%83%D9%85%D8%A9-%D9%81%D9%8A-%D9%87%D8%AC%D8%B1-%D8%A7%D9%87%D9%84-%D8%A7%D9%84%D8%A8%D8%AF%D8%B9-%D9%88%D8%A7%D9%84%D9%85%D8%B9%D8%A7%D8%B5%D9%8A
  • Imechapishwa: 18/05/2020