Swali: Bwana mmoja alitaka kugawa pesa kwa watoto wake. Je, ampe mtoto wa kiume mara mbili ya mtoto wa kike kwa vile Allaah (Ta´ala) amesema:

لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنثَيَيْنِ

“Mwanamume atastahiki mfano wa fungu la wanawake wawili.”[1]?

Au awagawie sawa kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mcheni Allaah na fanya uadilifu kati ya watoto wako.”[2]?

Kama atafanya hilo la kwanza kisha akafariki, kile walichopewa wavulana wapewe wasichana?

Jibu: Kwanza napenda kuuliza kama kile alichotoa ni matumizi au zawadi ya zaida.

Kama ni matumizi, basi atampa kila mtu kile anachohitaji, ni mamoja ni kidogo au ni kikubwa. Ikiwa mmoja katika watoto wa kiume anahitaji kuoa, atahudumia mambo yake ya ndoa na wala hawatowapa wengine mfano wake. Ikiwa mmoja wa wasichana atakuwa mgonjwa na akahitajia dawa za bei ya juu, basi atahudumia matibabu yake na wala hatowapa wengine.

Lakini ikiwa ni zawadi basi mtoto wa kiume anatakiwa kupewa mafungu ya wanawake wawili. Hakuna ugavi ambao ni adilifu zaidi kuliko wa Allaah (´Azza wa Jall). Akimpa mtoto wa kiume 100, basi ampe mtoto wa kike 50. Akifa kile alichopewa mtoto wa kiume hatopewa nacho mtoto wa kike. Kwa sababu hii ni haki na uadilifu kwamba mtoto wa kiume anapata mafungu ya wanawake wawili. Hadiyth inayosema:

“Mcheni Allaah na fanya uadilifu kati ya watoto wako.”

ina maana ya kufuata ule uadilifu uliojulishwa na Sunnah na Shari´ah. Huu ndio uadilifu.

Tunapasa kupambanua tofauti kati ya uadilifu na usawa. Hii leo watu wengi wanasema kuwa Uislamu ni dini ya usawa. Hili ni kosa. Ndani ya Qur-aan hakuna neno lolote linalojulisha usawa au kwamba watu wote wanalingana. Sehemu kubwa ya Qur-aan inapinga usawa:

لَا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِّنَ الَّذِينَ أَنفَقُوا مِن بَعْدُ وَقَاتَلُوا ۚ وَكُلًّا وَعَدَ اللَّـهُ الْحُسْنَىٰ

“Halingani sawa miongoni mwenu aliyejitolea kabla ya u shindi [wa ufunguzi wa mi wa Makkah] na akapigana, hao  watapata daraja kuu kabisa kuliko wale waliotoa baadae na wakapigana – na wote Allaah amewaahidi Pepo.”[3]

لَّا يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ غَيْرُ أُولِي الضَّرَرِ وَالْمُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ

“Hawawi sawa waumini wanaokaa [nyumbani] wasiokuwa na dharura na Mujaahiduun katika njia ya Allaah kwa mali zao na nafsi zao.”[4]

قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ

”Je, kipofu analingana sawa na mwenye kuona au viza vinalingana sawa na nuru?”[5]

Mara nyingi yaliyomo ndani ya Qur-aan yanapinga usawa. Qur-aan inazungumzia uadilifu:

إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ

“Hakika Allaah anaamrishia uadilifu na wemaa.”[6]

اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ

“Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na kumcha Allaah.”[7]

Kuna tofauti kati ya uadilifu na usawa. Lau tutatendea kazi udhahiri wa neno “usawa” basi tungesema kuwa mvulana na msichana wanatakiwa kupata sawasawa, kama yanavyoenezwa leo na watu wa propaganda. Lakini tukizungumzia uadilifu basi tutampa mtoto wa kiume kile anachostahiki na mtoto wa kike kile anachostahiki. Kwa ajili hiyo nataraji ndugu zetu waandishi na wengine kuzinduka juu ya jambo hili. Neno “usawa” limepenyezwa na baadhi ya watu. Sijui ni vipi waliliingiza. Kuna uwezekano ikawa ni kufahamu kimakosa, kuna uwezekano wakawa ni mikia ya makafiri. Dini ni ya uadilifu na uadilifu maana yake ni kumpa kila mmoja kile anachostahiki.

[1] 04:11

[2] al-Bukhaariy (2587).

[3] 57:10

[4] 04:95

[5] 13:16

[6] 16:90

[7] 05:08

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (13 A) Dakika: 27.44
  • Imechapishwa: 30/06/2021