Swali:

Muheshimiwa Shaykh Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn – Allaah akuhifadhi

السلام عليكم ورحمة الله وبركاته

Katika baadhi ya maeneo baada ya kuzikwa maiti basi husimama mmoja katika wahudhuriaji na akawaomba watu kuketi chini kisha anawatolea mawaidha mafupi akiwahimiza watu kulazimiana na dini. Baada ya hapo anamuombea du´aa yule maiti kwa sauti ya juu kisha wadhuhuriaji wanaitikia “Aamiyn” juu ya du´aa yake. Ni ipi hukumu ya kitendo hichi?

Jibu:

بسم الله الرحمن الرحيم

و عليكم السلام و رحمة الله و بركاته

Hayo yaliyotajwa katika swali ni Bid´ah iliyozuliwa ambayo haikuwa yenye kutambulika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kipindi cha Salaf. Imethibiti kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutahadharisha juu ya Bid´ah na kubainisha kwamba kila Bid´ah ni upotofu. Ni jambo lisilotambulika kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwawaidhi watu kabla wala baada ya maziko. Kubwa linaweza kusemwa juu ya maudhui hayo ni yale aliyopokea Imaam Ahmad na Abu Daawuud kutoka kwa al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Tulitoka pamoja na Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mazishi ya bwana mmoja kutoka katika Answaar. Tulipofika tukakuta mwanadani hajachimbwa. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaketi chini na sisi tukaketi pambizoni mwake. Ni kama kwamba walikuweko ndege juu ya vichwa vyetu. Mkononi alikuwa ameshika kijiti akipigapiga ardhini. Akainua kichwa na kusema: “Mtakeni ulinzi Allaah kutokamana na adhabu ya kaburi.” Alisema hivo mara mbili au mara tatu.”[1]

Kuhusu kumuombea du´aa maiti baada ya kuzikwa kwake, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya maziko alikuwa akisema:

“Muombeeni msamaha ndugu yenu na mumtakie uimara; kwani hivi sasa anahojiwa.”[2]

Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akiomba du´aa kwa sauti ya juu na huku watu wakiitikia “Aamiyn.” Hapana shaka yoyote kuwa uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Endapo kuna kheri katika mambo haya yaliyozuliwa basi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake wangeliyafanya kabla yetu. Kwa ajili hiyo ni lazima kwa ndugu zetu kutangamana juu ya waliohai na wafu wao kwa mujibu wa mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Alalah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia awali miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[3]

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[4]

Allaah atuwafikishe sote utakasifu katika nia na ufuataji, na atulinde kutokamana na fitina zilizo za wazi na zilizojificha. Kwani hakika Yeye ni mwenye kusikia du´aa.

Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

1418-03-13

[1] Ahmad (4/287) na Abu Daawuud (4751).

[2] Abu Daawuud (3221).

[3] 09:100

[4] 33:21

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Madjmuu´-ul-Fataawaa (17/398-399)
  • Imechapishwa: 23/06/2021