Swali: Kutokwa na damu puani au katika moja ya viungo vya mwili kunafunguza? Kudunga sindano kwenye mshipa au nyonga kunafunguza? Kutia dawa ya matone, kuwapaka wanja, kukusanya mate na kusukutua kwa ajili ya matibabu kunafunguza? Je, kuna kanuni yenye kuzingatiwa katika masuala haya?

Jibu: Yote haya hayamfunguzi mfungaji. Kanuni inasema kuwa hakuna ´ibaadah yoyote iliyowekwa katika Shari´ah inayoharibika pasi na dalili kutoka katika Qur-aan, Sunnah na maafikiano au kipimo sahihi. Tukiyatazama hayo mambo yote yaliyoulizwa, basi hatupati dalili inayokubalika ki-Shari´ah inayoonyesha kuwa swawm ya mfungaji inaharibika. Kujengea juu ya haya si halali kwetu kusema kuwa ´ibaadah yoyote ya mja imeharibika pasi na dalili. Lakini kuchezesha maji mdomoni ni kitu kimechukizwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia Laqiytw bin Swabirah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Fanya kishindo katika kuyapindisha maji puani isipokuwa ukiwa umefunga.”[1]

Ikiwa mtu anahitajia kusukutua na wala hawezi kuchelewesha mpaka wakati wa jua kuzama, basi inafaa kufanya hivo. Lakini hata hivyo anatakiwa kujichunga kwelikweli yasije kuingia tumboni mwake.

[1] Abu Daawuud (142), at-Tirmidhiy (788), an-Nasaa’iy (1/66) na Ibn Maajah (407).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/255-256)
  • Imechapishwa: 01/05/2021