Hajj Haisihi Kwa Kuacha Kumtembelea Shaykh Rabiy´ al-Madkhaliy?


Maneno haya yenye kutoka kwa huyu mwongo ni dalili ya wazi inayoonyesha upindaji. Upindaji wake ni wa wazi kabisa wenye kunuka. Ni wongo. Wongo huu uko wazi kabisa kwa kila mwenye kusikia maneno haya. Pamoja na hivo sisi tunamwambia kuwa kila pale ambapo Ahl-us-Sunnah wanakuja kwenye Misikiti miwili – Makkah na al-Madiynah – wamefanya hivo ili waweze kutekeleza ´ibaadah kubwa. Makkah wanaikusudia kutekeleza Hajj na ´Umrah. al-Madiynah wanaikusudia kutembelea Msikiti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo Swalah moja ni sawa na Swalah 1000 kwenye Misikiti mingine mbali na Msikiti Mtakatifu ambapo kuswali ndani yake ni sawa na Swalah 100.000. Baina ya nyumba yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na minbari yake kwenye Msikiti wake mtukufu ni moja miongoni mwa mabustani ya Peponi.

Tangu hapo zamani wanachuoni na waumini wenye kuja kwenye miji hii miwili na kutekeleza matendo haya mawili makubwa, lengo lao kubwa inakuwa ni kukutana na Ahl-us-Sunnah wal-Hadiyth. Wanasononeka lau wataijia, bali hata sehemu za miji mingine, baada ya mwanachuoni mashuhuri wa mji huu katika Ahl-us-Sunnah kufa. Abu Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

“Nilifika Baghdaad waliposema: “Jana alikufa ´Affaan bin al-Muslim.” Nilifika Basrah na wanasema: “Leo amekufa ´Uthmaan al-Mu´adhdhin.”

Ahl-us-Sunnah wanasononeka kwa kufa wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah katika mji wanaouendea. Imaam Abu Daawuud (Rahimahu Allaah) alifika Makkah na alikuwa anataka kupokea kutoka kwa watu wawili. Alifika katika mji mwaka wa 220 kwa ajili ya Hajj. Alikuwa anataka kukutana na ´Abdullaah bin Maslamah al-Qa´nabiy – mmoja katika wapokezi wakubwa na waaminifu wa “al-Muwattwa´” ya Imaam Maalik (Rahimahu Allaah). Allaah Akamuwafikisha kukutana naye na akapokea kutoka kwake. ´Abdullaah bin Maslamah akafa baada ya Hajj katikati ya Muharram mwaka wa 221. Wengine wakamsikilia wivu kwa kukutana na huyu Haafidhw bingwa ambaye alipokea “al-Muwattwa´” kutoka kwa Imaam Maalik na akapokea kwake. Kadhalika akapokea kutoka kwa wengine Makkah. Nukta muhimu ni kwamba wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah na Ahl-us-Sunnah wanafurahi wakifika Makkah kuhiji na baada ya hapo kukutana na wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah wal-Hadiyth.

Shaykh Rabiy´ ni miongoni mwa wanachuoni wakubwa wa Ahl-us-Sunnah wal-Hadiyth wa zama hizi. Hakuna haja ya kumzungumzia na himdi zote ni za Allaah. Hata maadui zake ambao wanamsemea uongo wanakiri kuwa ni mwanachuoni na amebobea vya kutosha katika suala hili. Hakuna shaka yoyote mwenye kutamka kwa namna hii anachokusudia ni kuwafanyia mzaha Salafiyyuun na Ahl-us-Sunnah na kuwachafua. Anachotaka ni kukimbiza watu na wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah. Sisi tunaazimia kwa yakini pasina kuwa na shaka yoyote ya kwamba yule mwenye kuwageuzia mgongo wanachuoni hawa wakubwa wa zamani – na Shaykh Rabiy´ na mfano wake leo – amepinda. Hawamchukii Shaykh Rabiy´ kwa sababu ya ushindaji wa maslahi ya kidunia. Wanamchukia kwa sababu analingania katika mfumo huu wa Salaf na kuwaraddi wenye kwenda kinyume. Hakuna kundi, pote au chama isipokuwa amewatwanga mshale wake kikwelikweli. Ndio maana wapinzani wake ni wengi. Kwa sababu ya wapinzani wake wote na kumzulia uongo ninamfananisha na Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab ambaye na yeye alikuwa na wapinzani wengi na kumsemea uongo sana. Walifikia kiasi cha kwamba waliwanasibisha watu na yeye na wakawaita “Wahhaabiyyah”. Hii leo mnawasikia wanasema “Madaakhilah” na “Jaamiyyah”. Sio jipya. Hapo zamani walisema “Hanaabilah”. Sio jipya. Hapo zamani Ahl-us-Sunnah walikuwa wanawaita “Hanaabilah”. Lengo lao ni kuwatukana. Wakati mwingine wanasema “Hashawiyyah”, “Mushabbihah” na “Mujassimah”. Kuna mfano mwingi wa maneno kama haya. Je, Hanaabilah hawakujinasibisha na mwingine asokuwa Ahmad bin Hanbal? Je, ni aibu kujinasibisha na madhehebu ya Ahmad (Rahimahu Allaah)? Ninaapa kwa Allaah sivyo, si mwingine isipokuwa Sunnah. Tunamhimidi Allaah kuifanya nchi yetu kuwa na madhehebu ya Ahmad bin Hanbal kwa njia ya ´Aqiydah, matawi, Sunnah, utenda kazi na kuwafuata Salaf. Imaam Ahmad ni Imaam wa Ahl-us-Sunnah kikamilifu. Tukinasibishwa naye sio aibu kwetu wala sio kitu kinachotuathiri. Tunajifakhari kwa hilo na himdi zote ni Zake Allaah.

Ibn Hanbal amekuwa ni mtihani wa kukusudiwa

kupitia Ahmad mtu anapata kumjua ni nani mwenye kushikamana [na haki]

Ukimuona mtu anayemponda Ahmad

basi jua kuwa atakuja kufichuka

Baada ya hapo ikahamia kwa Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah). Yeye, wanafunzi zake na masomo yake walitukanywa. Walifikwa na hili na lile. Wengi wenu mnajua jinsi Shaykh wao Shaykh-ul-Islaam Taqiyy-ud-Diyn Abul-´Abbaas bin Taymiyyah maudhi yaliyomfika. Pamoja na yote hayo Allaah Akaamua ashinde.

Halafu kukaja Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab. Akaudhiwa, akatengwa na kutimulia kwenye mji wake. Alishambuliwa na baadhi ya watoto wake wakauliwa vitani. Wakamzulia uongo. Allaah Amrahamu na Amridhie. Wakamzulia uongo na ulinganizi wake. Mpaka hii leo wanasema “Wahhaabiyyah”, lakini halimzidishii jengine isipokuwa kupata ushindi tu na himdi zote ni za Allaah. Anazidi tu kuwa wazi na kuwa juu ya kila mwenye kwenda kinyume naye. Allaah ndiye Analisimamia:

وَلَيَنصُرَنَّاللَّهُمَنيَنصُرُهُ

“Ndio, Allaah Atamnusuru yule mwenye kumnusuru.” (22:40)

Imaam huyu aliinusuru Dini ya haki ya Allaah na Da´wah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliotakasika na kusafika na Shirki na Bid´ah. Alipoona jinsi watu wamevotumbukia kwenye Shirki na Bid´ah akaanza kufanya kazi kwa bidii mpaka Allaah Akamtukuza na Akamfurahisha kwa kumfanya akaona jinsi watu wanavorudi katika Uislamu wa haki na Sunnah. Aliisafisha Dini hii na Shirki kubwa-kubwa na Bid´ah. Allaah Alimpa wanusuraji kutoka katika familia ya Su´uud – Allaah Awarahamu wote. Da´wah hii, ambayo ni mwendelezo wa Da´wah ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah ambayo ni mwendelezo wa Da´wah na madhehebu ya Ahmad bin Hanbal, ikashinda. Kwa mara nyingine Hanaabilah Ahl-us-Sunnah wal-Hadiyth wal-Athar wakashinda.

Kusini mwa Saudi Arabia Allaah Ametutunukia mujadidi mwingine wa kulingania katika Tawhiyd. Alikuja wakati mji ulikuwa umejaa Shirki na Bid´ah. Si mwingine isipokuwa ni mlinganiaji na mpambanaji Shaykh ´Abdullaah bin Muhammad al-Qar´aawiy (Rahimahu Allaah). Alitujia kusini mwa Saudi Arabia na Tawhiyd na Sunnah na kupambana na Shirki na Bid´ah. Alikuja akiwa mtu mmoja! Allaah Akaupa uhai Ummah mzima kupitia kwake. Salafiyyah ikaenea mno Jaazaan mwa kusini mwa Saudi Arabia. Baada ya kutokuwepo mafundisho kabisa akafungua masomo zaidi ya 2500. Haya mnayoona hii leo. Allaah Akamtunukia nchi hii ikamhifadhi, ikamsaidia na ikamnusuru wakati Da´wah yake ilipoanza kudhihiri. Watawala wa nchi hii wakasimama upande wake. Allaah Awajaze kheri. Mfalme ´Abdul-´Aziyz na Su´uud wote walifanya hivo. Alipata msaada mpaka pale ambapo Da´wah yake ilipobeba matunda.

Shaykh Rabiy´ ni mmoja katika matunda ya mtu huyu (Rahimahu Allaah). Mtu huyu ni mmoja katika matunda ya Da´wah ya Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab. Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab ni mmoja katika matunda ya Da´wah ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Shaykh-ul-Islaam ni mmoja katika matunda ya Da´wah ya Imaam Ahmad bin Hanbal. Ni mnyororo uliokamatana. Hakika mnajua fika kama mimi jinsi Shaykh Rabiy´ anavoinusuru Salafiyyah na ulinganizi katika Sunnah ndani ya nchi hii, nje yake na kila mahali, kwa uandishi na kuzungumza. Anafanya hivo kadiri na awezavyo. Pamoja na umri wake mkubwa ni Mujtahid wa hali ya juu katika uwanja huu. Hafikiwi na taarifa ya mwendaji kinyume isipokuwa anamraddi. Hii ni fadhila ya Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala) kwake. Je, hivi kweli mtu hapupii kukutana na mtu kama huyu? Ninaapa kwa Allaah mtu anapupia. Kwa sababu ni mmoja katika wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah leo. Wanaomraddi wanamraddi kwa batili. Tumeona jinsi wote hawa mwisho wao ulivokuwa. Huanza kuzungumza namna hii na halafu baadae wanarudi kwa al-Ikhwaan al-Muslimuun, mapote mengine na jumuiya [taasisi] za ki-Hizbiyyah. Jana walikuwa wakimuadhimisha na kumuheshimu Shaykh Rabiy´. Walikuwa wanasema kuwa maneno yake ni ya sawa. Hivi wamerudi kwao na kushuhudia juu ya nafsi zao upindaji. Hapo jana walikuwa pamoja naye. Hivi hali yao ni ile waliyokuwa wakiikemea hapo jana.

Hili bila ya shaka yoyote kama tulivyosema ni moja katika malengo makubwa ya mtu Salafiy na Sunniy, baada ya kutekeleza Hajj na ´Umrah, ya wajibu au iliyopendekezwa, kukutana na Shaykh huyu mtukufu anayeinusuru Dini ya Allaah kwa msimamo tunaoujua. Huu ni mtihani, haumdhuru kitu kama ambavyo haukuwadhuru waliokuwa kabla yake. Hadhuriki – kwa idhini ya Allaah – na wenye kukimbiza watu naye na kuchochea dhidi yake.

Kuhusiana na maneno ya kitoto na machafu kama haya mliyosikia, mnaweza kuyapelekea kwa Muislamu yeyote aliye na akili duniani na kumuuliza kuhusu yule mwenye kuhiji na hakumtembelea Shaykh Rabiy´ – Hajj yake sio sahihi? Mi nafikiri hata mwendawazimu hawezi kuingiwa [akilini mwake] na kitu kama hichi. Yote haya ni kuwachafua Salafiyyuun.

Mtu anapata mashaka juu ya yule mwenye kufika Makkah na akaacha kwenda kumtembelea Shaykh Rabiy´ pasina udhuru wowote. Roho ni maaskari walokusanyika. Zile zenye kujuana hufungamana na zile zisizojuana hutengana. Mtu Sunniy anampenda Sunniy mwenzake hata kama atakuwa upande mwingine wa dunia. Mmoja yuko magharibi na mwingine mashariki. Wanatamani kukutana na kuonana. Jitu la Bid´ah linamchukia Sunniy kama jinsi Sunniy analichukia jitu la Bid´ah. Hili halina shaka yoyote. Je, hivi kweli mtu hapupii kumtembelea Shaykh Rabiy´ ikiwa yuko Makkah na hana kizuizi chochote? Yeye ndiye mwenye kukosa. Halimdhuru kitu Shaykh Rabiy´. Yeye ndiye mwenye kukosa. Ahl-us-Sunnah wanashangazwa na kitu kama hichi. Yule mwenye kumgeuzia mgongo anajikosesha mwenyewe. Ni kama tulivyosema isipokuwa ikiwa kama hana udhuru wowote mfano wa familia ambayo hakuna mwingine awezae kuwaangalia, watoto, ufinyu wa muda na nyudhuru nyinginezo sahihi. Ama yule ambaye yuko Makkah wiki moja, siku kumi, na hawezi kumtembelea Shaykh Rabiy´ na kusema kuwa ni Salafiy… Eleza ni kitu gani kilichokuzuia. Hakuna sababu yoyote sahihi iliyomzuia. Hakuna shaka yoyote juu ya kwamba kuna kitu katika nafsi yake.

Isitoshe mtu anaweza kusema zaidi ya hayo, lakini hilo halimdhuru yeye wala halitudhuru sisi. Sisi ni Salafiyyuun kwa idhini ya Allaah. Huu ni uongo uliyoenea hii leo na kujulikana. Sio jipya. Ni la tokea zamani. Abul-Hasan na wafuasi wake walisema hivo. ´Aliy Hasan [al-Halabiy] na wafuasi wake walisema hivo. Hawa na mfano wao wataedelea. Hata hivyo ibara si lazima iwe moja. Inaweza kutofautiana. Baadhi inaweza kuwa laini kuliko nyingine. Pamoja na hivyo maana yake ni moja na lengo ni kuwachafua Salafiyyuun. Haya ndio malengo hata kama ibara zitatofautiana. Kuna mwenye kusema kuwa Hajj si sahihi. Mwingine anasema Hajj haitimii ikiwa hukumtembelea Shaykh Rabiy´. Mwingine anauliza kama Shaykh Rabiy´ ni moja katika nguzo za Hajj na ´Umrah na kadhalika. Miundo mbali mbali yenye maana kama hiyo. Makusudio ni kutaka kuwakimbiza watu na Shaykh na kumchafua kwa wale wenye kumpenda, kumtembelea, kwenda kwake na kumsikiliza. Lakini Allaah Amejaalia kuwepo kwa watu wenye kuvunja uongo huu kama jinsi Allaah Alivyojaalia kuwepo kwa watu wenye kuraddi uongo kwa Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab na Da´wah yake kama jinsi Allaah Alivyojaalia kuwepo kwa watu wenye kuraddi uongo kwa Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na Da´wah yake kama jinsi Allaah Alivyojaalia kuwepo kwa watu wenye kumtetea na kumhifadhi Imaam Ahmad na madhehebu na mfumo wake. Shaykh anapita katika njia ya watu hawa. Wanafunzi hujulikana kupitia waalimu zao. Ikiwa waalimu zao ni Ahl-ul-Bid´ah wanajulikana kupitia wao. Ikiwa waalimu zao ni Ahl-us-Sunnah wanajulikana kupitia wao. Tunamuomba Allaah (Jalla wa ´Alaa) Atuthibitishe sisi na nyinyi juu ya haki mpaka pale tutapokutana Naye.[1]

————
(1) Tazama http://firqatunnajia.com/sharti-ya-salafiyyah-kumtembelea-rabiy-al-madkhaliy/

  • Mhusika: Shaykh Muhammad bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.sahab.net/forums/index.php?showtopic=141445
  • Imechapishwa: 03/12/2014