Swali: Tatizo langu ni kuhusiana na mume wangu, ni mwanaume ambaye ana mapungufu katika Dini yake, haswali. Na pindi ninapomwita kuswali anakasirika na ananifanyia istihzai. Na anaendelea kuacha Swalah kwa hoja kuwa baba yake alikuwa haswali, hii ndio sababu na yeye haswali. Niliendelea na hali ya kumkumbusha na siku moja akanambia: “Ukiendelea kwa hali hii, mlango uko wazi”, hapo ndio nilifika namuomba Talaka. Na mara ya pili ilikuwa takriban sababu hiyo hiyo. Akanambia: “Usiniongeleshi mpaka siku ya Qiyaamah”. Ipi rai yako kwa mtu huyu na kwa maneno yake aliyosema kwa minasaba miwili, wa kwanza na wa pili? Je, huchukuliwa ni Talaka au nini? Na je, inajuzu kwangu kubaki nae katika hali hii?

Jibu: Mwanaume huyu haijuzu kubaki nae. Maadamu anaacha Swalah kama ulivyosema, kwa hilo anakuwa kafiri. Ikiwa baba yake naye haswali, kaiga kwake. Na wala haijuzu kumuiga kafiri asiyeswali, anatukana Dini, au anafanya kitu miongoni mwa vitu vinavyovunja Uislamu wa mtu au maasi katika maasi ya kumuasi Allaah. Watu wote hawa ni mamoja. Mwanaume huyu ni kafiri na kamuiga kafiri mwenzake kutokana na kauli yake. Na imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba kasema:

“Baina ya mtu na baina ya kufuru na Shirki ni kuacha Swalah.” (Kaipokea Muslim katika Swahiyh yake)

Na kasema (´alayhis-Swalaah was-Salaam):

“Ahadi iliopo baina yetu sisi na wao ni Swalah, mwenye kuiacha amekufuru.”

Kauli yenye nguvu katika kauli za wanachuoni ni kwamba, mwenye kuiacha kwa kuzembea na uvivu ni kafiri, hata kama hakupinga uwajibu wake. Na ikiwa mwanaume huyu anapinga uwajibu wake, ni kafiri kwa Ijmaa´. Kwa hali yoyote, mwanaume huyu ni mwanaume mbaya na ni kafiri kwa kuacha kwake Swalah kutokana na kauli yenye nguvu ya wanachuoni. Haijuzu kwako kubaki nae. Bali ni wajibu kwako kuachana nae na wala usimpe kitu. Na kauli yake kusema kuwa mlango uko wazi, hii ni kinaya. Ikiwa amekusudia Talaka, anakusudia utoke kwa nia ya Talaka, itakuwa ni Talaka. Na ikiwa hakukusudia Talaka, itakuwa sio Talaka. Lakini kwa hali yoyote, hata kama hakukutaliki, haitakikani kwako kubaki nae. Bali ni wajibu kwako kumuacha na umuachie [… sauti haiko wazi… ], na watoto wako uwachukue na yeye (mume) hana haki ya (kubaki na) watoto kutokana na ukafiri wake. Wewe ndiye aula zaidi ya watoto wako. Ni mwanaume mbaya kwa kumkufuru kwake Allaah (´Azza wa Jalla). Huenda Allaah Akamsamehe. Akitubu nawe bado ungali ndani ya eda, akarejea, akatubu kwa Allaah na akajuta kwa aliyoyafanya na akaanza kuswali, hakuna ubaya kwako kurudi kwake na maadamu ungali ndani ya eda. Ama baada ya eda hapana (kurudi kwake), isipokuwa kwa ndoa mpya.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alharamain.gov.sa/index.cfm?do=cms.scholarallsubjects&schid=8177
  • Imechapishwa: 27/01/2018