Haijuzu kuyaingiza maneno ya Allaah katika viumbe


Amesema (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Ni wa Allaah pekee ufalme wa mbingu na ardhi na vyote vilivyo baina yake; Anaumba atakacho na Allaah juu ya kila kitu ni muweza.” (05:17)

إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ ۖ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika mfano wa ‘Iysaa kwa Allaah ni kama mfano wa Aadam. Amemuumba kutokana na udongo kisha akamwambia: “Kuwa!” – na akawa.” (03:59)

Maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) ni sifa miongoni mwa sifa Zake. Allaah kwa sifa Zake ndiye muumba na kila kisichokuwa Yeye kimeumbwa. Ameviumba viumbe vyote kwa neno lake “Kuwa!” na vikawa kutokamana na maneno Yake. Kwa hivyo basi, haijuzu kuyaingiza katika jumla ya viumbe Wake kwa kuwa ni katika Sifa Zake. Kusema kuwa sifa miongoni mwa sifa ya Allaah imeumbwa ni ukafiri. Washirikina walimuomba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´aalyhi wa sallam) awasifie Mola Wao ambaye anawalingania wamuabudu Yeye peke yake. Ndipo Allaah akateremsha Suurah “al-Ikhlasw”:

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ اللَّـهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Sema: “Yeye ni Allaah Mmoja pekee. Allaah ambaye ndiye mkusudiwa haja zote. Hakuzaa na wala hakuzaliwa. Na wala hakuna yeyote anayelingana [wala kufanana] Naye.” (112:01-04)

Lakini, ndugu muheshimiwa, unajua ni wapi al-Khaliyliy alipotoa taarifu hii? Kama inavyosema ikidhihiri sababu basi kunaondoka kule kustaajabu. Ameichukua kutoka kwa watangulizi wake. Simaanishi wema waliotangulia (as-Salaf as-Swaalih). Ameichukua kutoka kwa Bishr al-Marriysiy Mu´taziliy ambaye al-Khaliyliy anajifakhirisha kuwa anafuata maoni yake inapokuja katika Qur-aan.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd al-Qawiym, uk. 194
  • Imechapishwa: 14/01/2017