Swali 10: Tunamuomba baba mlezi muheshimiwa neno kuhusu bay´ah juu ya watawala Saudi Arabia?

Jibu: Ni wajibu kwa waislamu wote katika nchi hii ya Saudi Arabia kusikiliza na kuwatii watawala kwa wema, kama zilivyofahamisha juu ya hilo Hadiyth Swahiyh zilizopokelewa na kuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haijuzu kwa yeyote kunyanyua mkono wake kutoka kwenye utiifu. Bali ni lazima kwa watu wote kusikiliza na kuwatii watawala kwa wema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kutoka ndani ya utiifu na akajitenga na mkusanyiko ambapo akafa, basi amekufa kifo cha kipindi cha kikafiri.”

Lililo lazima kwa muumini ni kusikiliza na kutii kwa wema na asitoke ndani ya usikizi na utiifu. Bali ni lazima kwake kunyenyekea na kujisalimisha juu ya yale yaliyosemwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Nchi hii ya Saudi Arabia ni ya Kiislamu na himdi zote njema anastahiki Allaah. Ni nchi inayoamrisha mema na kukemea maovu. Vilevile ni nchi inayoamrisha kuhukumiana kwa Shari´ah na kuihukumu kati ya waislamu. Kwa hivyo ni wajibu kwa raia wote kuisikiliza na kuitii kwa wema, kujichunga kutofanya uasi kwayo na kujichunga kuiasi. Kuhusu yule mwenye kuamrisha maasi, basi itambulike kuwa hakuna yeyote anayefaa kutiiwa kwayo. Ni mamoja mtu huyo ni mtawala au mwengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika si vyenginevyo utiifu ni katika wema. Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba.”

Kwa hivyo mtawala, raisi wa nchi, waziri, baba, mama au mwengineo akiamrisha maasi, kama mfano wa kunywa pombe au kula ribaa, basi haijuzu kumtii katika jambo hilo. Bali ni lazima kujiepusha na maasi hayo. Haifai kwa yeyote kuyadharau maasi. Allaah kutiiwa ndio jambo linalotangulizwa. Hakika si vyenginevyo utiifu unakuwa katika wema. Hivo ndivo ilivyokuja kusema Sunnah Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam ´Abdu-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa ´Ulamaa-ul-Kibaar fiy al-Irhaab wat-Tadmiyr, uk. 112
  • Imechapishwa: 27/02/2020