Haifai kuweka “In shaa Allaah” katika du´aa

Swali: Ni ipi hukumu ya mtu kuweka “Allaah akitaka” (إن شاء الله) katika du´aa yake?

Jibu: Haitakikani kwa mtu anapomuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) akaweka: “Allaah akitaka” katika maombi yake. Bali kinyume chake anatakiwa kuomba kwa matarajio na aadhimishe shauku. Kwani hakuna yeyote awezaye kumtenza nguvu Allaah. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

“Niombeni nitakuitikieni.”

Ameahidi kutuitikia. Kwa hivyo hakuna haja ya kusema: “Allaah akitaka”. Kwa kuwa Allaah anapomjaalia mja kumuomba basi anampa moja katika mambo yafuatayo:

1- Kumuitikia maombi yake.

2- Kumuepusha na shari kiasi chake.

3- Akamuwekea nayo kwa ajili ya siku ya Qiyaamah.

Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiseme mmoja wenu: “Ee Allaah! Nisamehe ukitaka. Ee Allaah! Nihurumie ukitaka. Bali anatakiwa kuomba kwa matarajio na aadhimishe shauku. Kwani Allaah hakuna wa kumtenza nguvu.”

Pengine mtu akauliza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si alikuwa akimwambia mgonjwa:

لا بأس طهور إن شاء الله

“Hakuna neno! [Ugonjwa] ni kusafishwa [na madhambi] akitaka Allaah”?

Ndio ni kweli amesema. Lakini kilicho dhahiri ni kwamba hakusema hivo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia ya kuomba. Alisema hivo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  kwa njia ya maelezo na matarajio. Kwa hivyo sio du´aa. Miongoni mwa adabu za maombi ni yule mwombaji aombe kwa matarajio.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (01/90)
  • Imechapishwa: 31/05/2017