03. Hadiyth “Kuleni daku…. “


Hadiyth ya tatu

3- Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuleni daku. Kwani katika kula daku kuna baraka.”

Maana ya kijumla:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaamrisha kula daku. Kula daku ni kula kula chakula na kunywa kabla ya kuingia alfajiri na mtu kujiandaa kwa ajili ya swawm. Kumetajwa hekima ya kiungu ambayo ni kupatikana kwa baraka. Baraka ndani yake mna manufaa ya kidunia na ya Aakhirah.

Katika baraka za daku ni ule msaada anaoupata mtu juu ya kumtii Allaah (Ta´ala) mchana. Kwani hakika yule ambaye yuko na njaa na kiu wanakuwa na uvivu juu ya ´ibaadah.

Katika baraka za daku ni kwamba yule mfungaji hachoki kule kutekeleza swawm tofauti na yule ambaye hakula daku. Mtu kama huyu anapata uzito na ugumu wa kuiendea.

Miongoni mwa baraka za daku ni kupata thawabu kwa kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Miongoni mwa baraka zake vilevile ni kwamba yule mla daku anaamka mwishoni mwa usiku ambapo anamdhukuru Allaah (Ta´ala), anamuomba msamaha kisha anaswali swalah ya Fajr kwa mkusanyiko. Hilo ni tofauti na yule ambaye hakuamka kula daku. Hili ni jambo limeonekana. Idadi ya watu wengi wanaoswali Fajr katika mkusanyiko Ramadhaan wengi wao ni kwa ajili ya daku.

Miongoni mwa baraka pia ni ´ibaadah ikiwa mla daku atanuia kujisaidia juu ya kumtii Allaah (Ta´ala) na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika Allaah katika Shari´ah Yake ana hekima na siri nyingi.

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Kupendekezwa kula daku na kutekeleza maamrisho ya Kishari´ah kwa kufanya hivo.

2- Haitakikani kuacha kula daku kutokana na zile baraka zinazopatikana ndani yake. Baraka inafasiriwa kwa kile kitendo cha kula na kile kinacholiwa daku. Hili halihesabiwi ni kulifasiri tamko moja juu ya maana nyingi tofauti. Bali hilo linafahamika kutokana na siyaaq ya  الفتح والضم.

3- Udhahiri wa amri hii ni uwajibu. Lakini kule kuthibiti Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufunga mpaka wakati wa daku kunapelekea amri hii kwenda katika mapendekezo.

4- Suufiyyah wanaona kuwa muda wa kula daku ni kama muda wa futari, jambo ambalo ni kuiondosha ile hekima ya funga. Nayo ni kuvunja yale matamanio ya chakula na kitendo cha ndoa. Hilo halipatikani isipokuwa kwa kupunguza chakula. Wako wengine ambao wamewajibu kwamba hekima ya funga sio kupunguza chakula na kinywaji. Bali hekima yake ni kutekeleza maamrisho ya Allaah (Ta´ala).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/317-318)
  • Imechapishwa: 15/05/2018