Hadiyth “Katika maneno ambayo watu waliyapata kutoka kwa Mitume… “

Imaam an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

20- Abu Mas’uud ‘Uqbah bin ‘Amr al-Answaariy al-Badriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Katika maneno ambayo watu waliyapata kutoka kwa Mitume wa mwanzo ni haya: “Ikiwa huna hayaa basi fanya utakalo.”

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ikiwa huna hayaa basi fanya utakalo.”

Wanachuoni wametofautiana katika kauli mbili:

1- Kauli ya kwanza kuna wanachuoni waliosema kuwa haya ni maamrisho. Hivyo maana ya Hadiyth inakuwa ikiwa jambo ambalo unataka kufanya sio katika mambo ya kuonewa hayaa, basi fanya utakalo miongoni mwa mambo hayo ambayo hayaonewi hayaa kati ya waumini. Kwa msemo mwingine ikiwa jambo sio haramu na sio katika mambo yanayoharibu tabia nzuri ya mtu, murua, ndani yake hakuna kuzembea au kupuuzia jambo la wajibu, sio katika mambo ya kuonewa hayaa katika Shari´ah, basi fanya utakalo na usijali kwa kuwa hii ni dalili ya kuonesha kuwa ni sawa. Hii ni kauli ya kundi katika wanachuoni ikiwa ni pamoja na Ishaaq, Ahmad na wanachuoni wengine wengi.

2- Kauli ya pili inasema kuwa sio maamrisho. Wanachuoni wenye kauli hii wana maelekezo aina mbili:

a) Jambo hili limetoka katika maana ya maamrisho ambayo ni kushikamana na kitendo na kwenda katika matishio.

“Ikiwa huna hayaa basi fanya utakalo.”

Bi maana ikiwa huna hayaa ya kujiepusha na haramu, maovu, kuzembea au kupuuzia mambo ya wajibu, basi fanya utakalo kwani asiyekuwa na hayaa hakuna kheri yoyote ndani yake. Hii itakuwa na maana imeenda katika matishio…

Maana yake ni kwamba ikiwa huna kizuizi kinachokuzuia na hayaa ambacho kinakuzuia na kuyakaribia maovu, basi fanya utakalo na utakutana na hesabu yako [huko mbele] na maovu ya kitendo hichi ambacho hakikukuzuia kwa hayaa.

b) Kuna jopo la wanachuoni waliosema kuwa hili limetoka katika matokeo ya maelezo. Bi maana kile kisichoonewa hayaa, basi watu hukifanya. Haya ni maelezo kuhusu watu na yale wanayoyafanya. Nayo ni kwamba yale mambo wasiyoyaonea hayaa huyafanya. Ikiwa huna hayaa kwa kitendo hicho, basi unapata kukifanya kwani watu [wengine] hukifanya. Udhahiri wake ni maamrisho na undani wake ni maelezo.

Kauli hizi mbili [zote] ziko wazi, kauli ya kwanza na ya pili. Bi maana kusema kuwa ni maamrisho au sio maamrisho au ni maelezo, limetoka katika matishio au maelezo, yote yako karibu [na usawa]. Hadiyth kuna uwezekano ikawa imeafikiana na kauli ya kwanza kama jinsi kuna uwezekano vilevile ikawa imeafikiana na kauli ya pili.

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Arba´iyn an-Nawawiyyah, uk. 299-301
  • Imechapishwa: 14/05/2020