2683- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Katika zama za mwisho watakuweko wanaume wenye kupanda juu ya viti vinavyofanana na kigoda cha ngamia. Watakuwa ni wenye kushuka kwenye milango ya misikiti na wanawake wao wamevaa lakini bado wako uchi. Vichwa vyao ni kama nundu ya ngamia. Walaanini, kwani hao wamelaaniwa! Lau baada yenu kungelikuja Ummah mwingine basi wanawake wenu wangeliwatumikia kama walivyowatumikieni wanawake wa watangu wenu.”

Ameipokea Ahmad (2/223), al-Mukhallasw katika ”al-Fawaa-id wal-Gharaa-ib al-Muntaqaat” (1/264 – asili), Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” (1454) na at-Twabaraaniy katika ”as-Swaghiyr” (232) na ”al-Awsatw” (9485).

Upokezi wa ´Abdullaah bin Wahb umekuja:

”Watakuwa ni wenye kupanda juu ya viti laini mpaka wanakuja kwenye milango ya misikiti.”

Ameipokea al-Haakim (4/436).

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaashiria usafiri wa sasa – magari. Magari zimewekwa viti laini na vizuri ambavyo vinakumbushia vigoda vya ngamia. Hilo linatiliwa nguvu na Hadiyth nyingine ambayo inaita usafiri wa kisasa kuwa ni “nyumba”, lakini baadaye imekuja kubainika kwamba kuna kukatika katika cheni ya wapokezi.

Katika Hadiyth kuna muujiza mwingine wa kielimu na wa kighaibu usiyohusiana na wale wanawake waliovaa lakini bado wako uchi, nao unahusiana na wale wanaume wanaopanda magari kwenda misikitini. Ninaapa kwa Allaah kwamba ni unabii wa kweli. Haya tunayaona kila siku ya ijumaa ambapo magari yanapaki karibu na milango ya misikiti mpaka njia zinakuwa zenye kubana. Wanaume wanashuka kutoka kwenye magari na wengi wao hawaswali swalah vipindi vitano. Angalau kwa uchache hawaziswali misikitini. Ni kama kwamba wamekinaika tu na swalah ya ijumaa na ndio maana wanamiminika kwa wingi. Pindi wanapopaki nje ya misikiti na kushuka kutoka kwenye magari yao hakudhihiri kwao athari yoyote ya swalah. Wala katika kutangamana na wake na wasichana zao. Kwa haki kabisa ni wanawake waliovaa lakini bado wako uchi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (6/1/415)
  • Imechapishwa: 28/06/2019