“Fanya kila kitu isipokuwa tendo la ndoa”

Swali: Ni nini kinachojuzu kutoka kwa mume juu ya mke wake siku za hedhi?

Jibu: Inafaa kwa mume kutoka kwa mke wake kila kitu isipokuwa tu jimaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanya kila kitu isipokuwa tendo la ndoa.”

Hapa ni pale alipoambiwa kwamba mayahudi hawawajamii wanawake siku za hedhi wakiwa majumbani. Kinachomaanishwa ni kwamba hawachanganyikani nao, hawatangamani nao na wala hawali pamoja nao. Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Fanya kila kitu isipokuwa tendo la ndoa.”

Allaah akateremsha kuhusu hayo:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ

“Wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara, hivyo basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike.”[1]

Bi maana jimaa. Ama kitendo cha yeye kulala naye kitanda kimoja, akambusu na akamvuta kwake ni mambo ambayo hayana ubaya. Kilichokatazwa ni jimaa peke yake. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuwa akinywa kwenye kikombe kisha anakichukua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na anaweka mdomo wake pahali alipoweka mdomo yeye ´Aishah. Pia akila mfupa na yeye akiuchukua na kuula. Yote haya kwa ajili ya kumfanya ahisi vizuri moyoni mwake, aanasike na kucheza naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 02:222

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa ad-Duruus https://binbaz.org.sa/fatwas/3688/%D9%85%D8%A7%D8%B0%D8%A7-%D9%8A%D8%AC%D9%88%D8%B2-%D9%84%D9%84%D8%B2%D9%88%D8%AC-%D9%85%D9%86-%D8%B2%D9%88%D8%AC%D8%AA%D9%87-%D8%A7%D9%8A%D8%A7%D9%85-%D8%A7%D9%84%D8%AD%D9%8A%D8%B6
  • Imechapishwa: 01/03/2020