Fadhilah za kufunga siku ya ´Arafah


1 – Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Inafuta dhambi za mwaka wa kabla yake na mingineyo.”[1]

Ameipokea Muslim, tamko ni lake, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy, Ibn Maajah na at-Tirmidhiy ambaye tamko lake linasema:

“ Swawm ya siku ya ´Arafah; hakika mimi natumai kwa Allaah atanifutia [dhambi za] mwaka wa baada yake na wa kabla yake.”[2]

2 – Vilevile Ibn Maajah amepokea kutoka kwa Qataadah bin an-Nu´maan ambaye amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Yule atakayefunga siku ya ´Arafah atasamehewa mwaka wa kabla yake na mwaka wa baada yake.”[3]

3 – Sahl bin Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefunga siku ya ´Arafah atasamehewa dhambi za miaka miwili mfululizo.”

Ameipokea Abu Ya´laa na wanamme wake ni wa al-Bukhaariy[4].

4 – Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameismulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayefunga siku ya ´Arafah, atasamehewa mwaka wa mbele yake na mwaka wa nyuma yake. Na yule atakayefunga ´Aashuuraa´, atasamehewa mwaka mmoja.”[5]

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Awsatw” kwa cheni ya wapokezi nzuri.

5 – Sa´iyd bin Jubayr amesema:

”Bwana mmoja alimuuliza ´Abdullaah bin ´Umar kuhusu funga ya siku ya ´Arafah. Akasema: ”Tulikuwa wakati tulipokuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukiizingatia ni swawm ya miaka miwili.”[6]

Ameipokea at-Twabaraaniy katika “al-Awsatw” kwa cheni ya wapokezi nzuri.

[1] Swahiyh.

[2] Swahiyh.

[3] Swahiyh kupitia zengine.

[4] Hivi ndivo alivosema. Katika cheni ya wapokezi yuko Abu Hafsw at-Twaa-ifiy na jina lake ni ´Abdus-Salaam bin Hafsw. Abu Daawuud ni mmoja katika wale watunzi sita waliopokea kutoka kwake. Ni mwaminifu.

[5] Swahiyh kupitia zingine.

[6] Nzuri kupitia zingine.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh at-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/590-591)
  • Imechapishwa: 06/07/2022
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy