Allaah amewateremshia mayahudi elimu yenye manufaa ambayo ni Tawraat. Ndani yake mna uongofu na nuru. Wakaipotosha na kubadilisha. Kwa sababu hawakutaki kuyatendea kazi maandiko ya Tawraat kama ambavo Allaah aliyateremsha kwa Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo wakaharibika na wakastahiki kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) hasira. Matokeo yake Allaah akawakasirikia kwa sababu walijua na hawakutendea kazi. Kwa ajili hiyo yule atakayejua katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) chochote kutoka katika mafunzo ya Qur-aan na Sunnah na asikitendee kazi, basi amejifananisha na wale waliokasirikiwa. Imepokelewa katika Hadiyth:

“Yule atakayejifananisha na watu basi yeye ni katika wao.”[1]

Maana yake ni kwamba anastahiki kuadhibiwa kama wao walivyostahiki kuadhibiwa. Adhabu ya kila mfanya jinai ni kutegemea na jarima yake na alivyoifanyia nafsi yake mwenyewe jinai.

Kwa hivyo kilicho cha lazima kwa muislamu aifuatishie elimu matendo. Kila pale atapofahamu masuala fulani miongoni mwa masuala ya Uislamu ayatendee kazi ili aweze kupata thawabu nyingi, atekeleze faradhi, atekeleze mambo ya wajibu na ajiepushe na mambo yaliyo ya haramu. Matendo yote hayo sababu yake ni elimu. Elimu ni ufunguo wa wema wote na ni mlango wa kheri zote. Mwenye kunyimwa elimu amenyimwa kheri zote.

[1] Abu Daawuud (04/44).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyq-ul-Wusuwl ilaa Idhwaah ath-Thalaathat-il-Usuwl, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 12/12/2019