Elimu ambayo ni lazima kwa kila muislamu kuijua

Swali: Je, kuna elimu ambayo ni lazima kwa waislamu wote kuijua?

Jibu: Ndio, ipo elimu ambayo ni lazima. Mosi kujua kuwa Allaah ndiye Mola na muumba wa kila kitu, kwamba Yeye pekee ndiye anastahiki kuabudiwa badala ya wengine, kwamba ametuumba sote ili tumwabudu, kwamba ametutumilizia Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuwa ni mwenye kutoa bishara njema na mwenye kuonya kama alivyowatuma Mitume wengine kabla yetu, kwamba Muhammad ndiye Nabii na Mtume wa mwisho na hakuna Nabii mwingine baada ya utume wake na hakuna Shari´ah nyingine baada ya Shari´ah yake, tunatakiwa kuitambua dini ya Uislamu kwa dalili zake na kwa nguzo zake tano; shahaadah, swalah, zakaah, swawm na kuhiji, na kwa nguzo za imani; kumwamini Allaah, Malaika Wake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar ya Allaah sawa ya kheri na shari yake, tuyajue hayo kwa haki, tulazimiane na kumtii Allaah. Aidha tunatakiwa kuwa na elimu ya mambo ya dini yetu, nguzo za Uislamu, nguzo za imani, namna ya kutangamana na mambo ya dunia yetu, elimu ya mambo ya halali na mambo ya haramu katika yale mambo ya dharurah kwetu ni mambo anayotakiwa kuyajua kila muislamu ili awe na utambuzi kuhusu dini yake.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalish-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.mufti.af.org.sa/ar/content/هل-هناك-علم-يجب-على-المسلمين-أن-يعرفوه-جميعاً؟
  • Imechapishwa: 12/06/2022