Du´aa kwa lugha mbali na kiarabu ndani ya swalah 02

Swali: Ni ipi hukumu ya kuomba du´aa ndani ya swalah kwa lugha isiyokuwa ya kiarabu khaswa ikiwa jambo hilo linafanywa na mtu ambaye hajui vizuri lugha ya kiarabu?

Jibu: Kuomba du´aa kwa lugha nyingine mbali na kiarabu kutoka kwa mtu asiyejua lugha ya kiarabu ni jambo linalojuzu. Ni mamoja ndani ya swalah au nje ya swalah. Kwa sababu mtu huyu asiyejua lugha ya kiarabu akilazimishwa kuomba du´aa kwa kiarabu itakuwa ni kumlazimisha kitu kisichokuwa ndani ya uwezo wake. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

Mtu pengine akiuliza ni kwa nini asifunzwe. Tunajibu kwa kusema tukimfunza matamshi asiyojua maana yake faida iko wapi?

Kwa hali yoyote kuomba du´aa inafaa kwa mtu akamuomba Allaah (Ta´ala) kwa lugha ya mwombaji. Ni mamoja lugha ya kiarabu au nyingine.

Kuhusu kusoma Qur-aan haijuzu kwa yeyote kuitamka isipokuwa kwa lugha ya kiarabu kwa hali zote.

Kuhusu Adhkaar zilizopokelewa akiwa na udhuru wa kujifunza nazo kwa lugha ya kiarabu hakuna neno akazisoma kwa lugha yake. Lakini kama mnavojua kwa mfano neno “Allaah” haiwezekani kulifasiri kwa lugha nyingine isiyokuwa ya kiarabu. Ikiwa haiwezekani basi aombe du´aa kwa lugha isiyokuwa ya kiarabu. Kwa hivyo vigawanyo ni vitatu:

1- Kuna mambo ambayo hayajuzu isipokuwa kwa kiarabu peke yake. Nayo ni usomaji wa Qur-aan.

2- Mambo yanayofaa kwa kiarabu na lugha nyingine kwa asiyejua kiarabu. Nayo ni kule kumuomba Allaah du´aa kwa yale ambayo hayakupokelewa.

3- Kuomba kwa du´aa zilizopokelewa, kama mfano wa Adhkaar na mfano wake, tunasema akiweza kuzisoma kwa kiarabu basi azisome kwa kiarabu. Asipoweza basi asome kwa lugha yake.

[1] 02:286

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.youtube.com/watch?v=CtCbCeme8LQ
  • Imechapishwa: 23/01/2020