Swali: Ni ipi hukumu ya doli za wasichana na vitabu vilivyo na picha vya wanyama na ndege? Watoto wanapenda kuvitazama na kujifunza kwa kule kuvitazama. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Doli kwa njia ya wanawake ziko aina mbili:

1- Doli ambazo zinajuzu na hazina neno. Doli hizo ni zile zisizokuwa na macho, pua na mdomo. Doli hizo hazina neno juu ya kufaa kwake. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuwa akicheza na doli aina hii.

2- Doli za plastiki ambazo zinakuwa kwa shakli ya mwanadamu mkamilifu. Doli hizo zina macho, midomo, kope na nyusi. Baadhi ya doli hizo pengine hata zikatembea na kutoa sauti. Doli kama hizi zinatakiwa kutazamwa vizuri. Lakini hata hivyo sitilii ugumu sana kwa sababu ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alikuwa na doli. Huenda kuna wasaa kwa msichana, khaswa kwa kuzingatia kwamba wanaburudika na kujishughulisha nazo. Lakini muda wa kuwa zipo doli nyenginezo, basi haitakiwi kuacha kitu kisichokuwa na mashaka na kukiendea kitu kilicho na mashaka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Achana na kile chenye kukutia mashaka na ukiendee kile kisichokutia mashaka.”

Kuhusu picha za wanyama wengine, kama mfano wa ngamia na simba, hakuna maana yoyote ya kuwa nazo. Mtu anaweza kutosheka nazo kwa picha za magari na matrekta. Mtoto huburudika navyo kama anavyoburudika na picha za viumbe wengine. Mtu akitenzwa nguvu kwa njia ya kwamba akapewa zawadi ya viumbe hivi vilivyo na picha, basi anatakiwa kuondosha kichwa chake na ibaki pasi na kichwa. Katika hali hiyo hakuna neno.

  • Mhusika: Imam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (26 A) Dakika: 12:40
  • Imechapishwa: 02/01/2021