Dhuhaa kila siku


Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kipenzi changu wa hali ya juu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliniusia mambo matatu: kufunga siku tatu za kila mwezi, Rak´ah mbili za dhuhaa na niswali Witr kabla ya kulala.”[1]

Wasia wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapomzungumzisha mmoja katika Ummah wake basi ni kwamba amezungumzisha Ummah mzima muda wa kuwa hakuna dalili inayoonyesha kinyume chake.

Kuhusu swalah ya dhuhaa kumepokelewa Hadiyth nyingi juu ya fadhilah zake. Hata hivyo wanachuoni wametofautiana kama imependekezwa kudumu kuiswali kila siku au kuiswali mara na kuacha mara nyingine. Maoni sahihi ni kwamba imependekezwa kudumu kuiswali kila siku kutokana na Hadiyth hii na nyenginezo. Hata hivyo hapana neno kwa yule ambaye ana mazowea ya kuamka usiku kuswali akaiacha baadhi ya nyakati. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila siku inayompambaukia mwanadamu basi kila kiungo chake cha mwili kinalazimika kutoa swadaqah. Kila Tasbiyh ni swadaqah, kila Tahmiyd ni swadaqah, kila Takbiyr ni swadaqah, kuamrisha mema ni swadaqah, kukataza maovu ni swadaqah na Rak´ah mbili anazoswali za dhuhaa zinamtosheleza na yote hayo.”[2]

Wanachuoni wanasema kuwa uchache wa swalah ya dhuhaa ni Rak´ah mbili na wingi wake ni Rak´ah nane. Wakati wake ni takribani dakika ishirini baada ya jua kuchomoza na takribani dakika tano mpaka kumi kabla ya jua kupondoka.

[1] al-Bukhaariy (1178), Muslim (721), at-Tirmidhiy (760), an-Nasaa’iy (1677), Abu Daawuud (1433) na Ahmad (7098, 7140 na 7409).

[2] al-Bukhaariy (2707) na Muslim (1009).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bahjat-ul-Abraar, uk. 85-86
  • Imechapishwa: 04/03/2021