Dhambi saba zenye kuangamiza


3- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Jiepusheni na dhambi saba zenye kuangamiza.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni yepi hayo?” Akasema: “Ni kumshirikisha Allaah, uchawi, kuiua nafsi ambayo Allaah kaiharamisha kuuliwa isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya mayatima, kukimbia siku ya vita na kuwazulia uongo wa kuzini wanawake waumini waghafilikaji na waliohifadhika.”

Kubwa katika hayo ni shirki. Kisha kunafuata uchawi kwa sababu mara nyingi unatokamana na shirki. Kwani uchawi una maana ya kuwaabudu majini na kuwaomba msaada na kujikurubisha kwao. Baada ya hapo kunafuatia kuiua nafsi ambayo imeharamishwa na Allaah isipokuwa kwa haki, riba, kukimbia siku ya vita ambapo yamekutana makundi mawili katika safu ana kwa ana ambapo mtu akalikimbia kundi lake na kuwatuhumu machafu wanawake waumini wenye kujihifadhi. Tuhuma hapa inahusiana na uchafu wa uzinzi.

Wameitwa waghafilikaji kwa sababu mara nyingi huwa hawatambui waliowatuhumu. Hukumu hiyohiyo inahusiana na wanaume wenye kujihifadhi. Hii ni dhambi kubwa. Mtuhumu anastahiki kusimamishiwa adhabu. Lakini hili mara nyingi linakuwa kwa wanawake. Ndio maana yule mwenye kuwatuhumu anatakiwa kuadhibiwa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 88-89
  • Imechapishwa: 09/12/2018