Damu inayotoka katikati ya meno wakati wa swawm na hukumu ya mate na makohozi

Swali: Katikati ya meno yangu natokwa na damu na yanaingia kinywani mwangu mchana wa Ramadhaan na khaswa wakati wa kuamka kutoka usingizini. Ni ipi hukumu ya damu hii kuingia kinywani mwangu? Je, inaharibu swawm yangu?

Jibu: Haiharibu swawm yako. Midhali hakuitambua na ikaingia bila ya kutaka kwake haiharibu swamw yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُم بِهِ وَلَـٰكِن مَّا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ

“Hapana dhambi juu yenu katika yale mliyoyakosea lakini isipokuwa katika yale yaliyokusudia nyoyo zenu.” (33:05)

Lakini mimi namshauri ndugu muulizaji kwa upande wa kitabibu, aende kwa madaktari wa meno na fizi ili atazamwe na wayatibu meno yake na ayasafishe siku zote. Akifanya hivo basi jambo hili litaisha kwa idhini ya Allaah.

Ajabu ni kuona niliulizwa swali ambalo nataka kuwapa nalo; naomba mnijibu: je, mtu inaharibika swawm yake kwa kumeza mate?

Mwanafunzi: Haiharibiki.

Ibn ´Uthaymiyn: Naomba ufafanuzi?

Mwanafunzi: Kuna watu wanaokusanya mate yao kisha wanayameza.

Ibn ´Uthaymiyn: Kwa hiyo unakusudia kwamba mtu akiyakusanya mate yake na kuyameza swawm yake inaharibika na asipofanya hivo swawm yake haiharibiki? Mimi nasema haiharibiki kwa njia zote hata kama mtu atakusanya na kuyameza. Lakini mimi nadhani kuwa hakuna yeyote anayekusanya mate yake na kuyameza. Baadhi ya watu wanapotoa makohozi ndio wanakusanya mate yao bila kukusudia, hili pia halifunguzi.

Wanachuoni wametofautiana juu ya makohozi kama swawm inaharibika au haiharibiki endapo yatafika kinywani mwake na akayameza. Kuna katika wao ambao wamesema kuwa yanafunguza. Kwa sababu makohozi sio mate ya kawaida. Kuna wengine wamesema kuwa hayafunguzi. Hapa ni pale ambapo tayari yameshafika kinywani. Ama yale makohozi ambayo yanahisiwa kooni na hayafiki kinywani hayafunguzi bila utatizi wowote.

Kwa ajili hiyo tunawakosoa baadhi ya watu wanapohisi makohozi tumboni mwao basi wanajaribu kuyavuta ili kuyatoa, jambo ambalo ni kosa. Yaache yashuke [tumboni yenyewe] hayaharibu swawm.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (41) http://binothaimeen.net/content/1611