Swali: Kuna aliyeandika kitabu kuhusu hukumu ya mwenye kuacha Swalah na kwamba sio kafiri. Miongoni mwa dalili alizotumia kuyatetea madhehebu yake ni kusema kwamba hakuna dalili ya Kishari´ah ya kwamba mpwekeshaji anatoka katika Uislamu kwa kitendo midhali haijatubainikia kuwa anapinga hata kama itakuwa baadhi ya yale Aliyoweka Allaah katika Shari´ah. Je, maneno haya ni ya Ahl-us-Sunnah au ni ya madhehebu yepi miongoni mwa madhehebu uliyotaja kuhusu imani?

Jibu: Sisi hatumkufurishi yeyote isipokuwa kwa dalili. Muislamu hatumkufurishi isipokuwa kwa dalili. Dalili zimeonyesha kuwa asiyeswali ni kafiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amebainisha kuwa asiyeswali ni kafiri. Dalili zimeonyesha kuwa asiyeswali ni kafiri. Ni kwa nini wajikakama? Je, wataka kumraddi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema:

“Baina ya mja na kufuru ni shirki ni kuacha Swalah.”

“Ahadi iliyopo baina yetu sisi na wao ni Swalah, yule mwenye kuiacha basi amekufuru.”

Ni kina nani “baina yetu sisi na wao”? Ni makafiri.

Ahadi iliyopo baina yetu sisi na wao ni Swalah, yule mwenye kuiacha amekuru, bi maana amekuwa ni katika wao. Kuna yaliyo wazi kuliko haya? Allaah (Jalla wa ´Alaa) Anasema:

فَلَا صَدَّقَ وَلَا صَلَّىٰ

“Hakusadikisha [hii Qur-aan] na wala hakuswali.”

Ameambatanisha kutokuswali na wakadhibishaji:

وَلَـٰكِن كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ

“Lakini [badala yake] alikadhibisha na akakengeuka.” (75:31-32)

Bi maana ameacha Swalah. Anasema (Subhaanahu wa Ta´ala):

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ

“[Watawauliza]: “Nini kilichokuingizeni katika [Moto wa] Saqar?”

yaani Motoni.

قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ

“Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali.” (74:42-43)

Jibu lao la kwanza wamesema:

قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ

“Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali.”

Ameambatanisha kutoswali na kuikadhibisha siku ya Qiyaamah. Mwenye kukadhibisha Qiyaamah anakufuru. Amesema tena (Ta´ala):

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wowote [ule] wa waombezi.” (74:48)

Walio mstari wa mbele ni wale wasioswali. Ni dalili inayoonyesha kuwa ni makafiri kwa kuwa muumini atapata uombezi wa waombeaji. Wale ambao hawatopata uombezi wa waombeaji ni makafiri.

Mtafutaji haki hutosheka na ile dalili ya kwanza tu. Ama yule mwenye kutaka mijadala, magomvi na kutetea watu wapotevu, huyu hatuna njia nyingine kwake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-is-Saffaariniyyah (08) http://www.alfawzan.af.org.sa/sites/default/files/sfranih_08.mp3
  • Imechapishwa: 22/06/2018